Image
Image

TANI TANO ZA MIRUNGI ZA KAMATWA SAME MKOANI KILIMANJARO ZIKISAFIRISHWA.

MORCE LYMO - MWENYEKITI WA TAJA, MWANDISHI WA MAKALA HII.
Katika kipindi cha miezi mitatu ya  Januari hadi Machi mwaka huu,  kiasi cha tani 5.2 za mirungi zilikamatwa zikisafirishwa maeneo mbalimbali hapa nchini. Hali hii inatisha, kwasababu ni kiasi kinacholingana na  mwaka mzima wa  2012 ambapo  tani 6.2 zilikamatwa.


Kwa takwimu hizo, inathibitisha kwamba  biashara ya mirungi inaendelea kuota mizizi siku hadi siku,  matokeo yake ni taifa kuwa na ongezeo la watu walioharibika kwa matumizi ya madawa za kulevya, ambapo mirungi mojawapo ya dawa hizo.

HII NI MITI YA MRUNGI IKIONEKANA HAPA, KATIKA KIJIJI CHA MHERO, KATIKA KIJIJI CHA MMENI KATA YA CHOME SAME( Picha na morice lymo). 
Hivi karibuni nilikuwa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kujionea hali  mbaya ya matumizi ya dawa hizo, kilimo huku  tatizo la rushwa `likitamalaki’ na kuwa kikwazo katika kutokomeza kilimo na biashara ya mirungi,
Kila unapopita  vijijini walalamikiwa wakubwa wa kukwamisha vita hiyo hudaiwa kuwa ni  baadhi ya askari polisi  kuwa `macho kengeza’ yaani hujifanya wanatekeleza sheria kwa kuwakamata watu wanaojishughulisha na mirungi huku wana tamaa ya pesa kwa kuwadai watuhumiwa `kitu kidogo’ wawaachie.


Hasira za wananchi  yanatokana na ukweli kwamba hushirikiana na viongozi wao kukomesha wahusika wa mirungi kwa kushirikiana na polisi, saa chache  unawaona watuhumiwa wakirandaranda mitaani, wakiendelea kuuza, kutafuna na wakulima wakiendelea kupanua mashamba.
MIRUNGI
Ninapozungumzia hali kuwa mbaya ni pamoja na katika kundi la watu 10, watu nane kati yao hutafuna mirungi, huku wasafirishaji wakubwa wakiwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda ambao nao hutafuna.


Nikiwa katika kijiji cha Mhero Kata ya Chome, nimeshuhudia baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakitafuna  wavulana kwa wasichana  wakitafuna mirungi  kwa kificho, na wanapomuona mtu ambaye hawamfahamu  humkimbia , hutema na kutupa  waliyoshikilia  kwa kisingizio cha kupoteza ushahidi.

Kupotea kwa imani ya wananchi dhidi ya askari polisi huchochewa na biashara ya mirungi kufanyika hadharani hasa  Hedaru  mjini, Same mjini na Makanya  ambako ni vituo vikuu vya wafanyabiashara .

Mathalani; Hedaru mjini na Makanya ambako wachuuzi wamekuwa wakitembeza kwa nyungo mitaani kwenye `vijiwe’, gereji, vituo cha mabasi,  migahawa  au majumbani kwa mtu mmoja mmoja wanayefahamu kuwa ni mtumiaji wa mirungi.
MIRUNGI IKIWA TAYARI KUINGIA SOKONI SAME.

Ni dhahiri kwamba  kwa takwimu ya watu nane kutumia mirungi kati ya watu 10, ingefanya  idadi kubwa ya watuhumiwa wa mirungi ikiwa askari polisi wangekuwa wanafanya kazi ipasavyo ya kutokomeza biashara, kilimo na utumiaji wa mirungi.

Kwa  mfano, haiingii akilini kwa idadi ndogo ya watuhumiwa 24 tu waliofikishwa mahakama ya Wilaya ya Same katika kipindi cha mwaka mzima wa 2012 hadi Aprili mwaka huu  kwa idadi hiyo ya walaji 8 kati ya 10, bado wanaosafirisha kwa boda boda, wachuuzi na wakulima. Bila shaka mahakama ingefurika washitakiwa wa mirungi!

Watuhumiwa wote hao waliachiwa huru baada ya kulipa faini na wengine kuachiwa huru bada ya mlalamikaji ambaye ni polisi kutofika `kuingia mitini’ na kutowasilisha vielelezo mahakamani.
BW. HERMAN CLEMENT - MKUU WA WILA YA YA SAME.
Ikumbukwe kwamba, mahakama hupotea watuhumiwa waliofikishwa mahakani na jeshi la polisi na mlalamikaji akiwa ni  Jeshi la Polisi kwa niaba ya Jamhuri. Kwa hiyo mahakama haiwezi kulaumiwa kwa idadi hiyo ya washitakiwa.

Takwimu hizo za mahakama, pamoja na polisi kufikisha watuhumiwa mahakamani na kasha kuingia mitini, kutopeleka vielelezo, kinawakera sio wananchi tu, pamoja na Mkuu wao wa Wilaya ,   Herman Clement Kapufi.

“Katika mambo ambayo yananikera ni idadi ndogo ya watuhumiwa wakati tatizo ni kubwa sana, watuhumiwa wanafikishwa mahakamani lakini vielelezo havipelekwi au walalamikaji kufika mahakani kutoa ushahidi kisha washitakiwa wanaachiwa huru..hii inajenga mazingira ya kuwalinda watuhumiwa na matokeo yake ni kushamiri kwa tatizo,”anasema DC Kapufi ambaye pia alionyeshwa kukerwa na kiwango kidogo cha faini.

Kwa hiyo katika mazingira kama hayo ni dhahiri kwamba malalamiko ya wananchi dhidi ya polisi yawe na mantiki kwasababu hiyo ni sawa na kesi ya ngedere kula mahindi kuipeleka kwa hakimu ambaye ni nyani!

Polisi wanatarajiwa kuwa watekelezaji, wasimamiaji wa sheria kwasababu wananchi wanawategemea  kuwa majemedari wa vita dhidi ya mirungi kwa hiyo pale ambapo jitihada za wananchi za kufichua maovu, jitihada hizo  ni dili kwa baadhi ya askari polisi, mwisho wake ni mirungi kuendelea kuuzwa  na kulimwa kama mchicha kwasababu wananchi watakata tamaa.

Napenda kuwaasa polisi wanaorudisha nyuma vita dhidi ya mirungi kwamba mwanazuoni mmoja kule Marekani, Robert Alan Dah ambaye ni mbobezi wa sayansi ya siasa, katika kitabu chake cha Theory and Methods of Political Science, aliwahi kusema “ Ni wajibu wa dola kuendesha juhudu za kutafuta suluhu za migogoro ya kijamii”.

Wajibu wa Polisi katika kadhia hii ni kutafuta mbinu za kijasusi bila tamaa, woga au hofu kuhakikisha inapata ufumbuzi wa tatizo la uzalishaji, usafirishaji na utumiaji wa mirungi wao wakitambua kwamba miti hiyo ni madawa ya kulevya,  kwa hiyo ni lazima polisi wakubali  dhamana zao na wajibu wao mbele ya jamii; kinyume na hayo ni  kutoitendea jamii haki na lazima wakubali kulaumiwa kwa namna  yoyote.

Kwa wenye macho hawaambiwi tazama, wale wachunguzi wa mambo wanaweza kuona kwamba kitendo cha polisi kufanya doria  kisha kukamata watu na mirungi kisha wanasema upelelezi haujakamilika wakati mtu amekamatwa na kielelezo inatia mashaka,

Kwamba ; hufanya doria wanawakamata watuhumiwa na kuwafungulia mashitaka mahakamani kisha polisi hawaendi kutoa ushahidi  hadi mahakama inamwachia huru mshitakiwa huleta mashaka.

Kwamba; polisi hufanya doria na kukamata na vielelezo (mirungi) kisha wanakaa navyo hawapeleki mahakamani  kama ushahidi wala hawatoi taarifa kuwa imeteketezwa, inaweza kuthibitisha malalmiko ya wananchi kuwa wapo wanawake wa askari  wanaopewa mirungi iliyokamatwa  na wanaume zao ili wakachuuze mitaani.

Ni dhahidi kwamba kwa idadi ya kesi  2,074 za mirungi na watuhumiwa 2,806 zilifunguliwa na kushitakiwa katika mahakama mbalimbali nchini katika kipindi cha 2001 hadi 2011, kitathimini ni chache  ukilinganisha na hali halisi na hivyo  kuleta hoja kwamba : Polisi ni `macho kengenza’ kudhibiti mirungi?

            Imetolewa na
Idara ya Habari, Elimu na Mawasiliano ya TTAJA
P. o. Box 77461, Tel: +255 754 865 959
Dar es salaam
Tanzania.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment