Jumuiya ya Maimamu
Zanzibar (JUMAZA) imelaani vikali kitendo
cha kumwagiwa maji yanayosadikiwa kuwa ni tindi kali raiya wawili wa
kike wa Uingereza katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar hivi karibuni.
Tamko hilo limetolewa
na Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Muhidin Zubeir Muhidini katika
ukumbi wa hoteli ya Mazson’s wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo.
Muhiddin
alisema kitendo cha kumwagiwa tindikali raia hao Kirstie Trup na
Katie Gee kina lengo la kuitia doa Zanzibar
ambayo inasifika kuwa ni kisiwa
cha amani na ukarimu wa kuwapokea vizuri wageni.
Aliwataka wazanzibari
kuendeleza ukarimu kwa wageni na kudumisha amani na utulivu, na
kutotoa mwanya kwa watu au vikundi vya watu vyenye nia mbaya ya kutaka kusababisha
mizozo kwa malengo yao binafsi na kuiharibu heshima ya Zanzibar.
Katibu huyo aliliomba Jeshi la Polisi nchini kufanya
uchunguzi wa kina na waharaka ili kubaini wahusika wa tukio hilo na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria .
Aidha aliliomba Jeshi
la Polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo kwa uadilifu
bila ya kupokea shinikizo kutoka sehemu yoyote ili ukweli
upatikane bila ya kuwadhuru watu wasiohisika na tukio hilo .
Sambamba
na tukio hilo JUMAZA imeshtushwa na tukio la kupigwa risasi Mhadhiri wa
dini ya kiislam Sheikh Issa Ponda huko Morogoro katika
mazingira ambayo hadi sasa yanaonekana kuwa na utata. .
Aidha alikemea vikali
kauli ya baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi , ambavyo
vinahusisha matukio ya aina hiyo na waumini wa dini ya Kiislamu.
Amesema vyombo
vya habari vinawajibu wa kutoa habari zilizo fanyiwa utafiti wa kina na kuacha
tabia ya kukurupuka kwa lengo la kutafuta umaarufu, huku
wakiliacha Taifa kwenye machafuko kama tunavyoshuhudia baadhi ya
nchi ulimwenguni.
“Vyombo vya habari
visiwe chanzo cha machafuko kwa kutoa taarifa zisizofanyiwa
uchunguzi na hatimae kusababisha machafuko,“ alisisitiza Katibu Mtendaji wa
JUMAZA..
Ameitaka Jamii ya Kimataifa kwa
upande wake kuwa waangalifu na taarifa zinazotolewa na baadhi ya
vyombo vya habari ambavyo lengo lake ni kuichafua Zanzibar
kimataifa.
Zanzibar yaleo.


0 comments:
Post a Comment