Mwenyekiti
Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akipongezwa na Mwenyekiti wa Bodi
anayemaliza muda wake wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Esther
Mkwizu (kulia), baada ya kuibuka mshindi wa kiti hicho cha uongozi katika
uchaguzi uliofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa mwaka wa taasisi hiyo
jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki. Aliyekaa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu na Makamu Mwenyekiti mpya
wa taasisi hiyo, Salum Shamte (wa pili kulia).
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa 14 wa
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) wamemchagua Dk. Reginald Mengi kuwa
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya taasisi hiyo katika uchaguzi uliofanyika mwishoni
mwa wiki.
Uchaguzi huo mkuu ulikuwa ni sehemu ya mkutano
mkuu wa mwaka ambapo taasisi hiyo ilitumia fursa hiyo kufanya uchaguzi wa
kupata bodi mpya baada ya bodi iliyokuwa ikiongozwa na Esther Mkwizu kumaliza
muda wake.
Uchaguzi huo ulioendeshwa kwa njia ya kura
ulisimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo.
Wajumbe wa mkutano mkuu waliopiga kura walikuwa
73 ambapo Dk. Reginald Mengi alipata kura 39 huku mgombea mwingine, Salum
Shamte akipata kura 34.
Hapakua na kura iliyoharibika.
“Kulingana na
sheria ya taasisi hii aliyepata kura nyingi anakuwa mwenyekiti mpya wa
bodi wakati aliyepata kura pungufu anakuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi,”
alisema Mapunjo alipokua akitangaza matokeo hayo.
Kwa maana hiyo, Salum Shamte anakua Makamu
Mwenyekiti mpya.
Viongozi hao wapya watahudumu katika nafasi hizo kwa muda wa
miaka miwili na baada ya kumaliza wanaweza kuingia katika uchaguzi tena kuomba
ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha pili.
Mkutano huo mkuu pia uliwachagua wajumbe 11
walioomba uongozi kupitia kongano wanazotoka ili kuwa wajumbe wa bodi hiyo.
Wajumbe wa bodi waliochaguli ni pamoja na
Deodatus Mwanyika atakaewakilisha sekta ya Nishati na Madini, Felix Mosha
(Uzalishaji/ Viwanda), Enock Dondole (vikundi vya biashara
mikoani), Anna Matinde (wajasirimali wanawake), Mbarouk Omar (Taasisi ya
Sekta Binafsi Zanzibar).
Wengine ni Peter Chisawillo
(Biashara), Salum Shamte (Kilimo), Gaudence Temu (Rasilimali na
Utalii), Dk. Gideon Kaunda (Makampuni), Dk. Charles Kimei (Benki na huduma za
kifedha) na Dk. Reginald Mengi (huduma).
Baada ya kutangazwa mshindi, Dk. Mengi alisema
katika kipindi chake atashirikiana na bodi na sekretarieti ya TPSF kuhakikisha
yale yote mazuri yaliyofanywa na uongozi uliopita yanaendelezwa.
“Tunahitaji kuzidi kuifanya sekta hii kuwa na
sauti moja na yenye nguvu ili iweze kushiriki vema katika uchumi wa nchi
yetu,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo ndiyo injini ya uchumi wa taifa.
Alitoa
changamoto kwa serikali kutumia fursa za rasirimali zilizopo nchini kwa kuwapa
kipaumbele Watanzania kwa ajili ya maslahi zaidi ya nchi kama zilivyofanya nchi
za Korea kusini na Malasia.
Pia alisema mataifa yote duniani yanaweka
kipaumbele zaidi kwa watu wake katika nyanja zote.
Akitoa mfano alisema kwasasa ambapo taifa
linaanza kuvuna rasirimali ya gesi na rasirimali nyingine, ni vyema vitalu
vitolewe kwa ajili ya kuvuna gesi baada ya kuwa sera inayoongoza uchimbaji huo
kupatikana.
“Ili nchi iweze kufaidika zaidi ni vyema
Watanzania wakapewa vitalu vya kuchimba gesi ili wakatafute wabia au fedha
kutoka taasisi za fedha za kimataifa kwa ajili ya kuvuna ili faida kubwa ibakie
nchini,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey
Simbeye alisema taasisi hiyo imepata kwa mara nyingine viongozi mahiri katika
nyanja ya masuala ya biashara na wenye ushawishi katika kuzungumza na serikali.
“Tunategemea bodi hii itazidi kuwa kichocheo na
tutazidi kufanya vizuri zaidi kutokana na uzoefu wa viongozi hawa na mafanikio
yatakuwa makubwa kwa faida ya taifa zima,” alisema.
TPSF ni taasisi ya sekta binafsi inayoundwa na
vyama vinavyowakilisha sekta binafsi mbalimbali nchini.
Wakati huo huo, serikali imesema itaendelea
kufanya kazi kwa karibu na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kama njia
ya kuimarisha sekta binafsi nchini na kuifanya kuwa injini ya ukuaji wa uchumi
na ustawi wa jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda katika mkutano mkuu wa 14 wa taasisi hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa nia ya serikali ni kuona kuwa taasisi
hiyo inashika hatamu katika uchumi wa nchi.
Alisema kuwa kwa muda wa miaka mitatu sasa
jtihada za makusudi za serikali na wadau wa sekta binafsi
zimeelekezwa katika kujenga sauti moja ya sekta binafsi Tanzania.
“Ni matumaini yangu kwamba taasisi yenu
itatekeleza majukumu yake ya msingi ya kutetea maslahi ya sekta binafsi na
kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta binafsi nchini kwa ufanisi
wa hali ya juu,” alisema.
“Ninafarijika kwamba tayari matunda ya jitihada
hizi yameanza kuonekana kwa kuweka mfumo madhubuti wa uongozi kwenye taasisi
yenu tofauti na ilivyokua awali,” alisema.


0 comments:
Post a Comment