Hatua hiyo inatokana na msimamo
wa wabunge wa vyama hivyo kususia mjadala wa muswada huo uliopitishwa hivi
karibuni na wabunge wachache wa CCM na Augustine Mrema wa TLP, wakidai
umechakachuliwa, huku Zanzibar ikiwa haijashirikishwa.
Kufuatia kusigana huko,
viongozi wa vyama hivyo; Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF)
na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walikutana na makundi mbalimbali ya wadau na
kutangaza kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kupinga rais asisaini
muswada huo.
Uamuzi wa wapinzani
hao uliwaibua mawaziri kadhaa, Stephen Wassira (Ofisi ya Rais-Mahusiano na
Uratibu), William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), Mathias Chikawe (Katiba na
Sheria) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wakiwabeza.
Mawaziri hao
walidai wapinzani wanapoteza muda wa mchakato ili rais awaite Ikulu tena kwa
mazungumzo waweze kunywa chai na juisi, jambo walilosisitiza kuwa haliwezekani,
kwani milango hiyo imefungwa.
Hata Waziri Chikawe
alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete, akisema kuwa asipousaini muswada huo
atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge, kwani lilifanya kazi yake kwa kufuata
Katiba.
Rais Kikwete
alitilia maanani hoja za pande zote na kuamua kuwaita wapinzani mezani
kuzungumza nao, akisema kuwa kama dhamira yao ni kutaka kupata Katiba mpya,
anawashauri waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia, bali watumie
njia halali, kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
Hoja zinazovutaniwa
Mbali na mambo
mengine, wapinzani wanadai kuwa muswada huo ulichomekwa baadhi ya vipengele
ambavyo vingeisaidia CCM kutawala mchakato mzima wa katiba.
Katika hoja ya
mapendekezo ya kumpa rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu, wapinzani
hao wanasema hayakubaliki, kwamba yanarudisha dhana kwamba wajumbe hawa
watakuwa watu wa rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
“Sheria iweke wazi
kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa’ na taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata
juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi.
“Sheria itaje
kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu watakaotokana na kila taasisi
iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa 354,” walisema wapinzani.
Katika suala la
Zanzibar, wapinzani hao wanasema wananchi wa huko hawakushirikishwa wakati wa
uandaaji wa muswada huo, hivyo kutaka mambo kadhaa yafanyike ili kuondoa
mgongano.
Kwamba, ili
kutimiza matakwa haya ya sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi
wa Zanzibar katika Bunge Maalumu.
Kwa mujibu wa
kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu
watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “...
haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.”
Hii ina maana
kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu ya Katiba
itakayojadiliwa na Bunge Maalumu inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke
yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo ya Muungano, ya
washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na
Katiba za washirika hao.
Rais Kikwete katika
kutambua hoja za wapinzani aliomba hekima ziwaongoze viongozi wa pande zote ili
waweze kutumia utaratibu walioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea
mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya
nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana
hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema
rais.
Aliongeza kuwa
kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na kutaliingiza taifa
kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Rais Kikwete
alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani bali katiba ya nchi,
katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko
wote.
Kuhusu ushiriki wa
Zanzibar, alisema kuwa alielezwa ni kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika muswada.
“Kama ni hivyo,
nashauri kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili wabunge walizungumze na
kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulaumiana
isivyostahili,” alisema.
Suala la Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nalo litakuwa sehemu ya mjadala huo, licha ya Rais Kikwete
naye kuona umuhimu wake akitaka ihusike kwenye hatua ya Bunge Maalumu.
“Nimeulizia
ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya serikali
wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo
la mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge
wengi.
“Nami naiona hoja
ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalumu, hasa wa kusaidia
kufafanua mapendekezo ya tume,” alisema. TANZANIA DAIMA.



0 comments:
Post a Comment