Image
Image

KATIKA MAISHA HAZIKOSI CHANGAMOTO,USIKATE TAMAA BADO NGUVU ZIPO.


 KATIKA maisha ni jambo la kawaida kupata misukosuko, makwazo, kuumizwa na mambo yanayofanana na hayo.

Kwa sababu tumeumbwa tofauti, wako walioumbwa kushughulika na maisha ya wenzao lakini siku zote uko mwisho wao, hivyo hupaswi kuruhusu wakukatishe tamaa.

Kwa nini nasema hivi, wako watu wamepitia magumu mengi katika maisha yao au wanapitia magumu, lakini wanapoyavuka haya, hawataki kuachilia na kusonga mbele, wanasahau kushughulika na maisha yao wanatazama ya nyuma.

Kwa wale waumini wa dini ya Kikristo, ndani ya Biblia kuna hadithi ya Yusufu ambaye aliuzwa na ndugu zake, baadaye alifungwa kwa kusingiziwa. Lakini hayo yote hayakumzuia kufanya kazi kwa bidii na kufikia ndoto zake.

Kama angetaka angewaweka ndugu zake waliomuuza moyoni, alikataa hilo hakuweka kinyongo na alipopata madaraka aliwasaidia na kuwatunza na hatusomi kuwa alilipiza kisasi mke wa Potifa.

Hali yake ya kuwa mfungwa haikumzuia kuja kutawala. Ndivyo hivyo hivyo kwako leo, maisha yako ya nyuma hayana nafasi katika maisha yako ya sasa na yajayo.

Eti kwa sababu umeishi kwa kuteseka sana, umenyanyasika, umesimangwa basi wewe uwe mnyonge na wa kusaidiwa tu, hapana. Kama bado uko hai una nafasi ya kuboresha maisha yako, haijalishi umepitia mapito na changamoto ngumu kiasi gani, kumbuka bado unayo maisha mbele yako.

Wako wanaobakia kulalamika kwa kutopelekwa shule na wazazi, wako waliopitia mikononi mwa mama wa kambo na kuteswa. Wako waliofelishwa na walimu, wako waliotengana na ndugu zao na kila aina ya changamoto za dunia hii lakini hayo yote ni mapito, ili mradi Mungu bado kakupa pumzi songambele usiyatazame hayo.

Sio wakati wa kulalama na kuacha kutumia fursa uliyonayo hata kama ni ndogo kuboresha maisha yako, kumbuka sio wewe peke yako kila mtu amepitia na anapitia matatizo na mitihani ya dunia hii iliyojaa kashikashi za kila aina.

Mazingira hayo magumu hayatupi kibali cha kulaumu wengine na kukosa furaha bila sababu. Kama ulianguka simama, anza kutembea na mwisho utakimbia, ni jambo la hatua na uvumilivu lakini zaidi ukiwa na dhamira ya kushughulika na maisha yako ili yalete maana.

Lakini ukiamini kuwa Mungu yupo upande wako daima utakuwa mwenye furaha, kuchangamka na mwenye matumaini. Kumbuka Mungu anaweza kukuinulia watu wa kukusaidia, na watu hao hawalazimiki kukusaidia hivyo chochote unachofanyiwa na mtu kipokee kwa moyo wa shukrani na kuzidi kumwangalia muumba wako.

Tena hapa wale wakatisha tamaa, wenye wivu na wasiopenda kuona mwingine anaishi maisha ya amani na furaha ndio wataibuka kwa vikundi kukusengenya, na kukusemea kila lililo baya, kwa sababu furaha yao ni kukuona ukiendelea kuteseka ama kunyanyasika.

Kumbuka kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji, kama una dhamira ya kushughulika na maisha yako na kuyafanya yenye maana hapa duniani, acha kusikiliza kelele za watu hao ambao mara nyingi ni wanakatisha wengine tamaa wakati wao wenyewe maisha yao matatizo matupu.

Unachotakiwa kufahamu ni kuwa kila mtu na maisha yake, tengeneza maisha yako kwa manufaa yako mwenyewe na sio kufurahisha wanadamu wengine wasiokuwa na shukrani na wala hawapendi kukuona ukifanikiwa katika maisha yako.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment