Image
Image

Serikali imesaini Azimio la Arusha linalohusu Kinga ya Jamii





Tanzania imepitisha Azimio linalohusu Kinga ya Jamii lenye msingi imara wa  kusimamia masuala hayo nchini na Afrika kwa ujumla ili kuwa na maendeleo halisi kwa watu wake.
Azimio hilo limepitishwa na kusainiwa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum kwa niaba ya Serikali jijini Arusha wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la siku tatu kuhusu Kinga ya Jamii ambalo lilishirikisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika.
Akitoa hotuba ya kufunga kongamano hilo Waziri Saada alisema kuwa maazimio yaliyofikiwa katika kongamano hilo yametoa mwelekeo na msingi wa kuimarisha kinga ya jamii kwa wananchi.
“Nafurahi kusema kongamano hili limekuwa hatua muhimu katika kutekeleza masuala ya kinga ya jamii kwa nchi zote washiriki wa kongamano hili na Afrika kwa ujumla” alisema Waziri Saada.
Waziri Saada alisema kuwa maazimio yaliyofikiwa wakati wa kongamano hilo jijini Arusha yanalenga kutumia mbinu mablimbali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu bora, afya, upatikanaji wa maji safi na salama.
Kutokana na malengo hayo, Serikali ya Tanzania iko mstari wa mbele katika kuwekeza na kusimamia  masuala ya kinga ya jamii kwa kuwa na bajeti endelevu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wanchi wake.
Akisoma Azimio hilo la Kinga ya Jamii, Katibu Mkuu Wazara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile alisema kuwa historia imejirudia ambapo yapata miaka 47 (1967-2014) iliyopita Tanzania ilipitisha Azimio la Arusha lililolenga kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini ambao Baba wa Taifa Mwl. Julius Kmbarage Nyerere aliwaita ni maadui wa taifa.
Maazimio mengine yaliyofikiwa katika kongamano hilo ni kupunguza umaskini na kukuza mitaji ya rasilimali watu ambapo Tanzania Bara inalenga ifikapo mwaka 2025 iweimepunguza tatizo la umaskini kwa watu wake wakati Tanzania na kwa upande wa Zanzibar inalenga kufikia hatua hiyo mwaka 2020.
Maazimio mengine ni kuwa utawala bora ambapo Tanzania imesisitiza kuendelea kuimarisha nguvu na sauti ya wananchi katika masuala ya kidemokrasia nchini na kutoa na kusimamia haki za watoto, wanawake na wanaume kwa kupinga ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, mimba za utotoni pamoja na uvamizi na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na mauaji ya wazee.
Kwa upande wake Muwakilishi wa UNICEF nchini Dkt. Jama Gulaid akitoa neno la shukrani aliisifu Tanzania kwa kuanza mapema kusimamia masuala ya kinga ya jamii ikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii na misaada inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wake wa kunusuru kaya maskini zilizo katika mazingira hatarishi.
Aidha,   Dkt. Gulaid aliipongeza Tanzania kwa kuwa na wimbo wa taifa unaozungumzia watu akiwataja kuwa ni wanawake, wanaume na watoto pamoja na bara la Afrika na watu wake licha ya kuwa na vivutio vizuri vya mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na visiwa vya karafuu.
“Wimbo huu wa Tanzania tofauti na nyimbo za nchi nyingine ambazo wao wanazungumzia askari, watumwa, watawala wakiwemo Malkia na Wafalme”alisema Dkt. Gulaid. 
Dkt. Gulaid aliwahakikishia wajumbe wa kongamano hilo kuwa wote wapo salama na wapo kwenye mpango wa kinga ya jamii kwa kuwa wametambuliwa na kubarikiwa na wimbo wa taifa wa Tanzania ambapo wajumbe waliimba wimbo huo na kuhitimisha kongamano hilo.
Kongamano hilo liliandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, Idara ya Kuondo Umaskini kwa kushirikiana na UNICEF, ILO, UNAIDS na EPRI ambapo washiriki wa konngamano hilo wanatoka katika nchi za Kenya, Uganda, Bangladesh, Afghanistan, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Afika Kusini, Ghana, Ethiopia, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment