Image
Image

Askari zaidi wamwagwa, Wahalifu wakimbilia msituni ingawa hali bado tete amboni tanga

Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda miongoni mwa wananchi huku askari wakiendelea kumiminika kwenda katika mapango ya Amboni yaliyopo nje kidogo na Jiji la Tanga kukabiliana na wahalifu wanaodaiwa kujificha kwenye mapango hayo.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa majira ya saa 5:00 asubuhi magari kadhaa yakiwamo ya kubebea wagonjwa (ambulance) yalionekana yakielekea kwenye mapango hayo.

Mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Karasha ambaye ni mtumishi mstaafu wa serikali ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kutokana na operesheni inayofanywa na vikosi hivyo tangu juzi, inadaiwa kuwa wahalifu wamekimbilia katika msitu wa Mbogo ambao upo kilometa chache kutoka mapango ya Amboni.

Wahalifu hao wamekuwa wakihisiwa na baadhi ya wananchi kuwa huenda ni magaidi.

Wakati hayo yakiendelea, wazungumzaji wakuu wa mamlaka za Serikali wamekuwa na usiri mkubwa wa kutoa maelezo kuhusiana na tukio hilo kama kuna watuhumiwa waliokamatwa.

JWTZ LANENA

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Joseph Masanja, akizungumza na NIPASHE jana, alisema jeshi hilo halihusiki na kutoa taarifa za tukio hilo kwa kuwa operesheni hiyo inafanywa na Jeshi la Polisi.

Meja Masanja alisema wanajeshi wanachokifanya katika operesheni hiyo ni kusaidiana na Jeshi la Polisi kupambana na wahalifu waliojificha katika mapango hayo.

“Operesheni inayofanywa Tanga ni ya polisi, siyo operesheni ya kijeshi, hata kama wanajeshi wameenda huko kusaidia, lakini JWTZ haliwezi kuhusika kutoa taarifa za kinachoendelea katika operesheni hiyo,” alisema.

RMO TANGA AGOMA 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu hali za askari waliojeruhiwa katika tukio hilo, alisema hawezi kuzungumza kwa sababu tukio hilo ni tofauti na matukio mengine.

“Mimi ni mtu ambaye napenda sana kushirikiana na waandishi wa habari, lakini tukio hili lipo tofauti kidogo na mengine hasa kutokana na suala la usalama, hivyo siwezi kukueleza hao majeruhi wanaendeleaje,” alisema.

Juzi askari sita waliokwenda eneo la tukio walijeruhiwa kwa risasi na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga-Bombo.

Tangu askari hao walipolazwa katika hospitali hiyo, mamlaka kadhaa zimezuia watu kwenda katika wodi ya Galanosi kuwaona wagonjwa huku maofisa kadhaa wa usalama wakiwa wametanda katika katika jengo la wodi hiyo kuhakikisha hakuna mtu anayeingia.

RC TANGA KUTOA  TAARIFA LEO

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula (pichani), akizungumza na NIPASHE alisema leo atatoa taarifa ya kinachoendelea kuhusiana na tukio hilo.

“Nimepigiwa simu na waandishi wengi na nimewaeleza kuwa siwezi kuzungumza lolote hadi kesho (leo) nitatoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kuhusu kinachoendelea,” alisema.

BULIMBA: BADO HAKUNA JIPYA

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alipoulizwa alisema bado hakuna habari mpya kuhusiana na tukio hilo zaidi ya taarifa zilizotolewa juzi.

“Wasilianeni na RPC Tanga, lakini kimsingi, bado hakuna jipya, taarifa tuliyoitoa jana (juzi), hakuna kilichoongezeka,” alisema.

CHAGONJA

Naye Mkurugenzi wa Opereshi na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja, ambaye yupo eneo la tukio alipotafutwa simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema bosi wake yupo kwenye kikao.

Kamshina Chagonja alipotafutwa tena simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na baadaye ikazimwa.  

Mapigano ya askari na kikundi cha uhalifu katika mapango ya Amboni yalianza Ijumaa na  kusababisha kifo cha askari mmoja na wengine sita kujeruhiwa wakati wakirushiana risasi na kikundi hicho chenye silaha za kivita.

Kufuatia mapigano hayo, wakazi wa Jiji la Tanga walieleza hofu yao na kupingana vikali na kauli ya Jeshi la Polisi na kwamba bado hali ya usalama kwao ni tete. 

Wananchi hao walieleza kuwa kinachowapa hofu ni mgongano wa kauli za jeshi hilo katika tukio hilo wakati Kamishna Chagonja alipokuwa akilizunguzia kwenye vyombo vya habari kwamba waliarifiwa kwamba silaha za moto zikiwamo walizoporwa askari Januari 26 zimefichwa ndani ya mapango, lakini kilichokutwa ni silaha za jadi yakiwamo mapanga, pinde na mishale pamoja na vifaa vya kutengeneza milipuko. 

Elizabeth  Mhagama, mkazi wa kijiji cha Amboni, alisema licha ya Kamishna Chagonja kuwataka wakazi wa Jiji la Tanga kutulia kwa kuwa hali ya usalama imeimarishwa, bado  wanayo mashaka na hofu kubwa kuhusu tamko hilo kulingana na mazingira yalivyo. 

Mhagama  alisema wanashindwa kuielewa taarifa hiyo  kwa sababu bado kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa kuwa wahalifu hawajakamatwa, hivyo hawajulikani ni kundi gani, limetoka wapi na lilikuwa na lengo gani. 

“Tunaliuliza Jeshi la Polisi kikundi hicho ni cha watu gani, je kinatokea wapi, kina nguvu kiasi gani hadi kufanikiwa kujeruhi vibaya askari na kisha kutoroka?” alihoji Mhagama.

Naye  Ally Shaban, mkazi wa Kijiji cha Kongwa jirani na lilipotokea tukio hilo,  alilitaka Jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu mwendelezo wa matukio ya uhalifu wa kutumia silaha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi na kutokamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo. 

Janathan Joseph, mkazi wa  Majimoto, alisema mbali na tukio la juzi yapo matukio mengine yakiwamo yaliyosababisha mauaji kwa raia ambao walivamiwa na kuporwa mali na kuwa licha ya watuhumiwa kushindwa kupatikana, lakini hakuna taarifa za mwendelezo wa kushughulikiwa kwa matukio hayo. 

Joseph alitoa mfano wa tukio la watu waliyojeruhiwa na bomu la kutupwa kwa mkono kwenye banda la video la kijiji cha Amboni mwanzoni wa mwaka huu ambako watu kadhaa walijeruhiwa na mmoja kati yao kupoteza maisha, lakini hakuna aliyekamatwa. 

“Yapo matukio mengi kama la mfanyabishara wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe ambaye  alivamiwa na kuuawa kwa risasi kabla ya kuporwa mali,  tukio la utekaji wa gari eneo la Michungwani wilayani Handeni baada ya kuwekewa magogo barabarani…yote haya hakuna kitu,” alisema Mariam Mdoe. 

Walielezea tukio la uporaji wa silaha  na  kusema kitendo cha askari polisi kunyang’anywa SMG mbili zenye risasi 60 kwenye kibanda cha chips hivi karibuni jijini Tanga wakiwa doria ni fedheha.  

CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment