Image
Image

Kesi ya Mwangosi yavuta shahidi wa tatu

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, leo inatarajia kuendelea kusikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten, Daud Mwangosi, inayomkabili aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pacificus Cleofas Simon.

 Ni baada ya mashahidi wawili kutoa ushahidi katika Mahakama hiyo Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita mbele ya Jaji Paulo Kihwelo.

 Jaji Kihwelo leo anatarajia kusikiliza ushahidi wa shahidi wa tatu katika  kesi hiyo ambaye hata hivyo, hakutajwa.

Jaji huyo wiki iliyopita aliamuru upande wa utetezi kupokea kielelezo cha gazeti la Septemba 3, mwaka 2012 kama utambuzi wa awali ili kusaidia ushahidi wa keshi hiyo.

Jaji Kihwelo alisema kuwa kielelezo hicho ni muhimu kwa sababu kitasaidia kutumika katika ushahidi wa kesi hiyo ya mauaji ya mwandishi huyo.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Said Mnunka ambaye ni Ofisa mstaafu wa FFU, alidai kuwa hakumtambua aliyedaiwa kufanya mauaji hayo hadi alipotazama picha kwenye gazeti.

“Sikuweza kutambua chochote kuna kitu kilitokea, lakini  kama Septemba 3, niliona gazeti ofisini kwa RPC wa Mkoa wa Iringa,  Michael Kamuhanda, ndipo nilibaini kuwa kuna kitu kilitokea jana yake (Septemba 2) baadaye ndipo tulizifuatilia kwa mtu mmoja mmoja kuanzia kwa wale askari walionekana kwenye ile picha hadi  kumbaini mtuhumiwa,” alidai Mnunka

Naye Shahidi namba mbili katika kesi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya (OCD) cha  Mufindi mkoani Iringa,  Assel  Mwampamba, alidai kuwa Septemba 1, mwaka 2012,  alipigiwa simu  na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,  Michael Kamuhanda, na kumuamuru aandae kikosi kwenda Kijiji cha Nyololo kuzuia maandamano na mkutano wa Chama cha Demokraasia na Maendeleo (Chadema).

“Siku hiyo nilitekeleza maagizo kama nilivyoagizwa na RPC kesho  (Septemba 2) tulielekea Nyololo nikiwa na kikosi changu, gari la mkoa moja, magari mawili ya  askari wa FFU kutoka mjini Dodoma,” alidai.

OCD Mwampamba aliendelea kudai kuwa walipofika Mufindi walikutana na magari mawili ya polisi kutoka Wilaya ya Mufindi na kuelekea kwenye eneo la  tukio.

 Alidai walipofika Kijiji cha Nyololo walikuta Chadema wamefunga vinasa sauti kwa ajili ya kuanza mkutano wao na kwamba aliteremka kwenye gari na  kuongea na viongozi wa chama hicho, lakini walikaidi na kutamka kuwa  liwalo na liwe lazima wafanye mkutano wao.

Alidai kuwa aliamriwa kuzuia maandamano hayo ili kutekeleza amri ya Serikali baada ya kutangaza kuzuia vyama vyote vya siasa  visiendelee na mikutano kutokana na zoezi la sensa ya watu na makazi.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kuona fujo zimetulia,  ndipo waliamriwa kuingia kwenye magari kwa ajili ya kurudi kwenye kambi zao. 

Hata hivyo, alidai kabla hawajaondoka, alishtukia Mwangosi  ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, amemkamata  mikono bila kujua sababu, ndipo alipoamua kupiga yowe kuomba msaada.

Alidai wakati askari wakienda kumsaidia, alisikia mlipuko wa kishindo na  kupoteza fahamu.

Alidai alipozinduka alijikuta amelazwa Hospitali ya Wilaya Mufindi akipatiwa matibabu bila kujua kilichotokea Septemba 2, mwaka 2012.

Alidai badaye aliambiwa kuwa Mwangosi alifariki  dunia. “Sikujua mwandishi huyo alikuwa na dhumuni gani, ndiyo maana nikaamua kuomba msaada kutoka kwa askari wenzangu ili waweze kunisaidia, ” alidai Mwampamba.

Jaji  Kihwelo aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapoendelea kusikiliza ushahidi huo.

Jaji Kihwelo alisema kuwa mashahidi hao wawili watahitajika mahakamani hapo kama ushahidi walioutoa haujakamilika.

Baada ya shahidi wa pili kumaliza kutoa ushahidi, Jaji Kihwelo alisema kuwa shauri hilo limehairishwa na hakumtaja ni shahidi yupi atatoa ushahidi leo.

Awali Wakili wa Serikali, Sunday  Hyre,  alidai kuwa Septemba 2, mwaka 2012, mtuhumiwa huyo alidaiwa kumuua Mwangosi kwa kumpiga kwa  bomu kwa makusudi, lakini mtuhumiwa alikana shitaka hilo.                           

Alidai kuwa mauaji hayo yalitokea Septemba 2 mwaka 2012 katika  kijiji cha Nyololo  wakati  Chadema wanajiandaa kwa ajili ya kufanya maandamano na mkutano mkubwa pamoja na kufungua tawi la chama.

Mtuhumiwa huyo anatetewa na Wakili Rwezaula Kaijage.


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment