Image
Image

UKAWA wamtaka Rais Kikwete kumaliza mda wake akiiacha nchi salama bila Machafuko


UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umemtaka Rais Jakaya Kikwete, ahakikishe anamaliza muda wake wa uongozi salama pasipo kuiacha nchi kwenye machafuko kwa kushinikiza upatikanaji wa Katiba Mpya na matumizi ya mfumo mpya wa uandikishaji wapigakura kwa njia ya kielektroniki (BVR), wakati hakuna maandalizi ya kutosha.

Viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, walitoa tamko hilo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakielezea athari zinazoweza kutokea kutokana na Serikali ya Rais Kikwete,kushinikiza matumizi ya BVR na kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.

Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alisema kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya ni wazi kwamba shinikizo la kulazimisha wananchi kuandikishwa kwa mfumo wa BVR, linaweza kuiacha nchi kwenye machafuko.

Alisema shinikizo hilo linatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani chama hicho, ndicho kinanufaika na BVR; na kwamba UKAWA tayari ilishaweka msimamo wa kutoshiriki kupiga kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa.

"Ili Rais Kikwete aiache nchi katika amani yake na kuepuka machafuko ni vyema aache kushinikiza masuala hayo, asubiri amalize muda wake wa miaka 10 kuliko kuendelea kushinikiza wananchi kutumia BVR huku wananchi wengine wakiwa hawana taarifa na nini kinachoendelea kuhusiana na uandikishwaji kwa kutumia mfumo huo," alisema Mbowe.

Alisisitiza kwamba lazima ieleweke kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haina fedha, lakini pia Sheria inahitaji NEC kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura angalau mara mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu mwingine unaofuata.

"Lakini kwa makusudi Serikali ya Rais Kikwete imevunja sheria ya kuboresha daftari hilo," alisema na kuongeza;

"Kitendo hiki kina malengo mabaya ya kutaka kuongeza muda wa utawala wake kwa kisingizio kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika kwa datari hilo ambalo halijaboreshwa," alisema Mbowe.

Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema juzi uongozi wa UKAWA ulipata taarifa kuhusiana na hali inayoendelea Makambako, mkoani Njombe ambako uandikishaji wa majaribio unafanyika.

Alisema katika uandikishaji huo wa majaribio mifumo ya BVR imeshindwa kufanya kazi hali inayochangiwa kutokuwepo kwa maandalizi kwa watendaji wake.

"Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kutoka kwa viongozi wetu walioko eneo la uandikishaji wa wapigakura, mfumo huo ulifeli kabla ya kuzinduliwa rasmi juzi na Waziri Mkuu na kupigiwa chapuo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi," alisema Prof. Lipumba.

Alitaja maeneo ambako mfumo huo umeonesha kufeli kuwa ni NEC kutokuwa na watumishi wa kufanya kazi hiyo na kupuuza ushauri wa mwelekezi kutoka Marekani.

Alisema mtaalamu huyo alishauri NEC iwe na watumishi zaidi 10,000 kwa ajili   ya kufanikisha uandikishaji huo nchi nzima,lakini haikufanyika hivyo.

Lakini pia alisema watumishi wa NEC walioanza kufanya kazi mkoani Njombe wamepatiwa elimu kwa muda wa siku moja tu kabla ya zoezi hilo kuanza na huku wengine wakiwa hawajui hata kushika kamera.

Alisema matatizo yaliyojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapigakura yanaonesha wazi kuwa Daftari la Wapigakura halitakamilika ili litumiwe katika zoezi la kura ya maoni.

"Ni vyema Rais Kikwete akakubali ukweli huu. Suala la kura ya maoni liahirishwe mpaka baada ya uchaguzi," alisema na kuongeza; " Tatizo kubwa zaidi ni kuwa Tume kushindwa kuandikisha wapigakura wote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa sababu mashine za kuandikisha wapigakura zina hitilafu."


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment