Image
Image

Kenya, Nigeria zagoma kuiazima Tanzania BVR

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo zilikataa.

Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.

Kitendo hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee uandikishaji unaendelea kufanyika ambako utamalizika Aprili 12, 2015.

“Tulitaka kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:

“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”

Kuhusu mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema: “Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”

Katika uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Katika mahojiano maalumu na viongozi, wahariri na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen makao makuu ya kampuni hiyo Tabata Relini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, NEC ilianza mchakato huo bila vifaa ikitegemea kuazima.

“Tulipokwenda Kenya na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania) kuangalia walivyofanikisha mchakato huo wakatueleza kuwa NEC walikuja hapa kuazima BVR za kuandikisha... tulikuwa na mawaziri pale yaani ilikuwa aibu na walitueleza kama hadi Novemba hamjanunua hamuwezi kuandikisha. Walisema walikuwa na BVR 15,000 Kenya na waliandikisha wapiga kura milioni 14 kwa zaidi ya siku 45 hadi 60, sisi tuna matatizo, matatizo.

“Wanatupa wasiwasi mkubwa, ikiwa lengo ni kuandikisha wapiga kura wote haiwezekani tukawa na kura ya maoni Aprili 30, lakini ukiwa unahitaji lazima uandikishe kwanza halafu ufanyike uhakiki wake, lakini muda huo hautoshi?

Kauli hiyo ya Profesa Lipumba kuhusu kusimamishwa kwa kura ya maoni pia ilitolewa Februari 12 na viongozi wa vyama 22 vya siasa walipokutana na NEC kujadili mchakato huo wa uandikishaji kwa kutumia BVR.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Mchakato huu ni muhimu na kama hautafanyika vizuri tutaichafua nchi yetu. Wadau washirikishwe na waridhike kwani kusipokuwa na uwazi kutaleta shida huko mbele.”
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment