Image
Image

Nani wa kuiwakilisha Ukawa urais 2015?

Ni takriban miezi minne sasa tangu vyama vinne vya upinzani nchini kupitia ushirikiano wao walioupa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kusaini makubaliano ya kushirikiana pamoja na kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo.

Umoja huo unaoundwa na vyama CUF, Chadema, NCCR- Mageuzi na NLD, unakabiliwa na kazi moja ngumu ya kufikia mwafaka wa kumpata mgombea urais, kabla filimbi ya uchaguzi kupulizwa.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanasema kabla ya kumpata mgombea mmoja, vyama hivyo vinne, vitalazimika kufanya uamuzi katika sera zao kabla ya kuja na jibu la mgombea kutoka chama kimojawapo atakayekuwa na sifa ya kupeperusha bendera kwa niaba ya umoja huo.

Kufikia hatua hiyo, changamoto kubwa inayoukabili umoja huo ni namna ya kumpata mgombea wa urais atakayetoa upinzani mkubwa zaidi kwa mgombea wa chama tawala.

Historia ya wanaoweza kugombea

Mpaka sasa aliyekuwa mgombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010 kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye anayeonekana kuwa anaweza  kupata mtaji mkubwa wa kura.

Matarajio haya yanahanikizwa na  takwimu za uchaguzi wa mwaka huo zinazoonyesha kuwa ndiye aliyepata kura nyingi kulinganisha na wagombea wa vyama vingine vitatu ambavyo mwaka huu vimeamua kujiunga pamoja kupitia Ukawa. Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Dk Slaa alipata asilimia 26.34 ya kura zote na kuweka rekodi ya upinzani ikilinganishwa na wagombea wengine miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya Ukawa waliowawahi kugombea siku za nyuma.

Kwa CUF kuna kila dalili kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anaweza kupendekezwa kugombea kiti cha urais kupitia Ukawa. Mgombea huyu si mgeni katika chaguzi, ameshiriki tangu mwaka 1995 bila ya mafanikio.

Katika chaguzi nne zilizopita CUF kupitia Profesa Lipumba kimekuwa katika mtiririko usioridhisha wa kupanda na kushuka katika upataji wa kura za wananchi.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995,  alipata kura 418,973, sawa na  asilimia 6.43 ya kura zote na kushika nafasi ya tatu akiwa nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustine Mrema aliyegombea kwa tiketi ya  NCCR- Mageuzi.

Profesa Lipumba aliingia tena katika uchaguzi wa mwaka 2000 na kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,329,007 (sawa na asilimia 16.26) akiwa nyuma ya Mkapa na uchaguzi uliofuata alipata kura 1,327,125 (sawa na asilimia 11.68) kabla ya kushuka tena mwaka 2010 alipopata kura 695,667 (asilimia 8.06).

Kigogo mwingine wa Ukawa ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia. Hata hivyo,  hajaonekana kuleta upinzani kwani hana historia ya kugombea urais, licha ya kuwa chama chake kimepata kusimamisha mgombea wa nafasi  mara tatu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment