Image
Image

Hotuba ya Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania kwenye maadhimisho ya siku ya mwalimu nyerere (Nyerere Day) na uzinduzi wa program maalumu ya uongozi na maadili ya chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere, jumatatu tarehe 13 aprili, 2015 kivukoni-dar es salaam


Hotuba ya mhe. Dkt. Jakaya mrisho kikwete, rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania kwenye maadhimisho ya siku ya mwalimu nyerere (nyerere day) na uzinduzi wa program maalumu ya uongozi na maadili ya chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere, jumatatu tarehe 13 aprili, 2015 kivukoni-dar es salaam.
Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi; 
Mhe. Meck Said Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam; 
Mhe.  Bi Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Temeke; 
Mheshimiwa Dkt. Terezya Huvisa, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo;

Prof. Shadrack S. Mwakalila, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere; 
Mheshimiwa Pius Msekwa, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;

Waheshimiwa Mabalozi;

Ndugu Wanataaluma na Wafanyakazi Waendeshaji wa Chuo;

Ndugu Wanafunzi;

Ndugu Wanajumuiya ya Chuo;

Ndugu Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

Mheshimiwa Waziri wa Elimu, 
Ninakushukuru sana Mheshimiwa  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na pamoja na Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kivukoni kwa kunialika Chuoni hapa siku ya leo.  Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa busara wa kuanzisha Programu Maalum ya Mafunzo ya Uongozi na kuizindua leo tarehe 13 Aprili, 2015 siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  miaka 93 iliyopita. 

Pongezi kwa Chuo cha Kumbukumbu ya

Mwalimu Nyerere

Ndugu Wageni Waalikwa;

Nakupongeza sana Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo, Mkuu wa Chuo, wakufunzi na wafanyakakazi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya na kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana hapa Chuoni.  Katika miaka 10 ya uhai wake Chuo kimekua sana.  Kama alivyoeleza Mkuu wa Chuo, mmefungua tawi kule Zanzibar na sasa mnadahili wanafunzi 4,000 hapa Kivukoni na 2,400 kule Zanzibar. Aidha mnaendesha mafunzo ya ngazi za awali (foundation), cheti, stashahada na shahada hapa Kivukoni na katika Tawi la Zanzibar. Nawapongeza sana kwa upanuzi huu mkubwa. 
Programu ya Uongozi na Maadili

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nakosa maneno mazuri ya kuelezea furaha yangu kwa uamuzi wenu wa kuanzisha Programu Maalum ya Uongozi na Maadili. Nafurahi kuwa mnafanya moja ya mambo muhimu yaliyokuwa yanafanywa na Chuo cha Kivukoni wakati ule kabla ya kuwa Chuo cha Sayansi ya Jamii cha Kivukoni na sasa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. 

Napenda mjue kwamba hapa palikuwa hoteli iliyoitwa Ghana Hotel.  Mwaka 1961, hoteli hiyo ilinunuliwa na kuanzishwa Chuo cha Kivukoni ambacho madhumuni yake ni kuwaendeleza kwa elimu na mafunzo vijana wa kiafrika ambao hawakupata elimu nzuri.  Walengwa hasa walikuwa vijana waliojiunga na harakati za kudai uhuru ili waweze kujiendeleza maishani.  Miongoni mwa wanufaikaji ni pamoja na hayati Kighoma Malima ambaye aliacha shule darasa la 10 na kushiriki harakati za kudai Uhuru.  Alikuja Chuoni hapo akaendelezwa na baadaye kwenda Marekani kusoma zaidi na hata kufikia kuwa mchumi bingwa aliyetambulika kimataifa. 

Chuo kilianza kwa kufundisha masomo ya sayansi ya jamii na walimu wake walikuwa wa kutoka nje hususan Uingereza, Canada na Marekani.  Ilikuwa hivyo kwa sababu wasomi wazalendo walikuwa wachache sana.  Baadaye ndipo walipoajiriwa kidogo kidogo mpaka hatimaye wazungu walipoondoka.

Baada ya Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere aliagiza Chuo kifundishe Azimio hilo kwa viongozi wa Chama na Serikali.  Mwaka 1972  Chuo kikabadilika kabisa na kuwa cha mafunzo ya siasa na uongozi.  Kwa ajili hiyo, viongozi wa ngazi mbalimbali wa Chama wakati ule, Serikali na taasisi zake wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama na mashirika ya umma walipitia Kivukoni.  Walipatiwa mafunzo ya siasa,  ya uongozi maadili.  Mimi ni mmoja wa wanafunzi waliopitia na kuhitimu katika Chuo hiki.  Lengo lilikuwa ni kuwawezesha kuwa viongozi wanaoweza kutimiza ipasavyo majukumu yao uongozi katika taifa linalojitegemea na la kijamaa.  Viongozi pia ambao ni waadilifu wanaotambua na kuheshimu miiko ya uongozi.  Katika mafunzo yale miiko ya uongozi kwa mujibu wa Azimio la Arusha yalikuwa yanafundishwa.

Baada ya mageuzi ya kiuchumi na ya kisiasa, na Chama cha Mapinduzi kuachana na vyuo vya siasa, kukatokea ombwe kubwa kwa upande wa mafunzo ya uongozi.  Si vyema kuhoji busara ya uamuzi wa Chama lakini athari zake sote tunaziona.  Kumekuwepo na kilio na manung’uniko kuhusu maadili na mienendo ya viongozi. Tumeshuhudia viongozi wakifanya matendo ya utovu wa maadili na hata kutumia lugha zisizofanana na uongozi ulio adilifu. Hivyo, uamuzi wenu huu umekuja wakati mwafaka sana.  Ni uamuzi uliokuja wakati unahitajika sana. 

Mkuu wa Chuo;

Mabibi na Mabwana;

Wanazuoni wamekuwa na mjadala kwa karne nyingi kuhusu uongozi na hayajakamilika.  Moja ya mambo yanayowashughulisha wanazuoni ni kama viongozi huzaliwa na vipaji vya uongozi au huandaliwa kwa mafunzo kuwa  viongozi. Huu ni mjadala unaoendelea hata sasa katika fani ya sayansi ya siasa. Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa pamoja na kuwepo ushahidi kuwa wako viongozi wenye kuzaliwa na vipawa na karama za uongozi, hata hivyo, ubora wa viongozi, hata kwa wale waliozaliwa na vipawa na karama zao hutokana na mafunzo.  Inaweza kuwa mafunzo darasani au kwa kuona na kwa kutenda.  Bahati mbaya hatuna vyuo vya uongozi wa jamii.

Mafunzo kwa viongozi ni muhimu kwa kuwa huwapa nyenzo na ufunguo wa kuyaelewa mazingira wanayoongozea, historia na uzoefu wa eneo wanaloliongoza, watu wanaowaongoza, matarajio yao, hulka zao, changamoto zao na muhimu sana maadili na miiko ya uongozi wenyewe. Hali kadhalika, uadilifu katika uongozi, hujumuisha desturi na tabia zinazokubalika na zinazotarajiwa na jamii na wananchi kutoka kwa kiongozi. Wananchi hawamtegemei kiongozi kuwa mla rushwa, mlevi, mhuni, mwongo au asiye na uhusiano mzuri na watu.

 Maadili na miiko ya uongozi vinapaswa kuzingatiwa na viongozi wote katika jamii na taifa bila ya kujali vyama vya siasa.  Kiongozi asiye na uelewa huu, hupwaya katika uongozi. Maadili na miiko ya uongozi ni tunu muhimu sana kwa kiongozi yeyote. Kiongozi anapaswa awe mtu mwenye uadilifu usiotiliwa shaka utakaomfanya aaminiwe na awe na  mamlaka ya kimadili (moral authority) juu ya wale anaowaongoza.

Katika miaka hii 10, tumejishughulisha sana na masuala ya maadili katika uongozi na utendaji Serikalini. Tumefanikiwa kuimarisha mifumo ya kusimamia maadili ya viongozi kwa kutunga Sheria, Kanuni na Taasisi za kufuatilia mienendo ya viongozi. Tumeimarisha Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuipa uwezo wa kiuchunguzi, rasilimali watu na vitendea kazi. Tumelipa meno Baraza la Maadili na tumeliona kwa mara ya kwanza likiwaita na kuwahoji viongozi wenye tuhuma za kimaadili.

Mwaka 2009 tumetunga Sheria Mpya ya Rushwa iliyoboreshwa na kuongeza nguvu kupambana na rushwa.  Orodha ya makosa ya rushwa imeongezwe kutoka manne hadi 24 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeimarishwa kwa majengo, vifaa na rasilimali watu. Hivi sasa TAKUKURU iko katika wilaya zote nchini na watuhumiwa wengi wa rushwa wamefikishwa katika mahakama na fedha nyingi zimekuwa zinaokolewa. 

Vilevile, tumetunga Sheria ya Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi ili kuhakikisha kwamba maadili ya kupata viongozi wa kuchaguliwa katika taifa letu yanazingatiwa. Tutakapokamilisha Sheria ya kutenganisha shughuli za siasa na biashara tutakuwa tumepiga hatua kubwa.  Tumetunga pia Sheria mpya ambayo imeimarisha Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).  Imesaidia kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuwabana viongozi na watumishi wa umma wanaofanya vitendo vya wizi au ubadhilifu wa fedha na mali za umma.  Yote haya tumeyafanya ili kuimarisha mifumo ya kusimamia maadili ya viongozi na watendaji wetu.

 Bahati nzuri katika Katiba Inayopendekezwa, Bunge Maalumu la Katiba limesisitiza na kuweka uzito unaostahili kwa maadili ya viongozi na watendaji wa umma.   Ibara 28 na 29 inazungumzia maadili ya viongozi wa umma, na ibara 30 na 31 inazungumzia maadili ya watendaji wa umma.  Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa tutakuwa tumefanikiwa sana katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maadili nchini.  Ombwe lililoachwa na Azimio la Zanzibar kuhusu miiko ya uongozi litakuwa limepata jawabu la uhakika.   

 Ni ukweli usiopingika kuwa pamoja na jitihada hizo, leo hii tunayo nakisi ya maadili miongoni mwa viongozi na watendaji wa umma.  Funzo tunalolipata hapa ni kuwa kukinga ni bora kuliko kutibu. Mifumo ya udhibiti pamoja na umuhimu wake, si badala ya mifumo ya kuwaandaa viongozi kimaadili. Zamani kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Chuo cha Kivukoni zilikuwa sifa muhimu za kupata uteuzi wa uongozi wa siasa.  Baada ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa na kuingia kwa mfumo wa soko huria na vyama vingi, mambo hayo hayakupewa umuhimu.  JKT ikadorora, vijana wakakosa fursa ya kujengwa uzalendo.  Ukichanganya na Azimio la Zanzibar lililolegeza miiko ya uongozi ya Azimio la Arusha, kumekuwa na mmong’onyoko mkubwa wa maadili miongoni mwa viongozi.  Kufa kwa Chuo cha Kivukoni kumeshusha ubora wa uongozi. 

Baada ya kurejesha JKT, hakika, taifa linahitaji sana programu ya aina hii tunayozindua leo ili kutuandalia viongozi wazuri, wenye mtazamo wa kitaifa na maadili mema. Nasema hivyo kwa kuwa sote ni mashuhuda wa matatizo ya maadili ya uongozi nchini.    

Hatuna budi kuwaandaa viongozi wetu hasa vijana kwa mafunzo maalumu ili waje kuwa viongozi bora. Ni jambo ambalo tulikuwa tukilifanya siku za nyuma. Uzoefu unaonyesha hata katika nchi zilizoendelea wanafanya hivi. Viko vyuo maalum vinavyoandaa na kutoa viongozi wa kada mbalimbali. Katika nchi za wenzetu kuna ngazi fulani za uongozi huwezi kushika ikiwa hujafundwa katika taasisi maalumu.  Kwa kuzingatia ukweli huo, ndiyo maana tumeanzisha Chuo cha Uongozi kiitwacho Uongozi Institute.  Chuo hiki kinalenga kutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Serikali.  Wamekuwa wakitoa mafunzo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.   

Nimefurahishwa na taarifa yako kuwa kutakuwa na Kada za aina tatu katika mafunzo ya program hii yaani ngazi ya juu yenye viongozi na watendaji wa  kitaifa na mkoa;ngazi ya kati itakayohusisha viongozi wa ngazi ya wilaya; na ngazi ya chini yenye viongozi wa ngazi za kijiji. Aidha, umesema yatakuwa ni mafunzo ya muda mfupi. Nakubaliana nanyi kwani si vyema kuziacha nafasi hizi wazi kwa muda mrefu. Vile vile, ni muhimu sana mafunzo haya yakaegemea pia katika vitendo na uzoefu badala ya nadharia pekee. Hii inajumuisha kuwa na wakufunzi mchanganyiko kutoka katika taaluma na wale kutoka katika uongozi na utendaji wa fani mbalimbali.

Uamuzi wenu wa kuanzisha Kibweta cha Mwalimu Nyerere kwa madhumuni ya kusimamia program ya mafunzo haya ni mzuri. Nimefurahishwa pia na uteuzi wenu wa Mheshimiwa Pius Msekwa kuwa Mwenyekiti wa Kibweta hiki. Chaguo hili ni muafaka kwani amesheheni historia, uzoefu na hazina kubwa ya uongozi. Ni imani yangu kuwa chini ya uongozi wake programu hii itafanikiwa. Sisi katika Serikali tunaahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano mtakaohitaji. Tuleteeni mapendekezo yenu kuhusu program hii ili ifanyiwe kazi na tuanze kuleta viongozi kwa ajili ya mafunzo hayo.

Changamoto za Chuo

Mkuu wa Chuo;

Kama ulivyoeleza, kukua na kupanuka kwa Chuo hiki kumekuja na changamoto zake. Idadi ya wanafunzi inaongezeka wakati majengo ya hosteli ni finyu. Umezungumzia ujenzi wa hosteli kusimama kutokana na uhaba wa fedha.  Nitawasaidia kusema.  Kuhusu kupewa majengo ya TAFICO ili myabadili matumizi na kuyatumia kwa kufundishia itabidi kushauriana na wenye majengo kujua mipango yao na mahali hapo.  Kama itawezekana tutawapeni taarifa.  Kuhusu tatizo la mmomonyoko wa fukwe unaotokana na kuongezeka kwa bahari tutawasiliana na mamlaka husika utafiti ufanywe na ushauri wa kitaalamu utolewe.

Nikuhakikishie kuwa nimepokea changamoto zenu na ni changamoto za msingi na tutatazama moja baada ya nyingine tuone namna ya kujenga Chuo hiki kulingana na mahitaji yake ya sasa na ya siku za usoni. 

Hitimisho

Mabibi na Mabwana;

Niwashukuru sana kwa kunialika katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere na ufunguzi wa Programu Maalum ya Uongozi na Maadili.  Nimefurahi sana kujumuika na nanyi wote katika eneo hili ambalo linanikumbusha nilipokuwa nikihudhuria mafunzo katika chuo hiki. Sasa ninayo furaha kutangaza kuwa Programu Maalum ya Mafunzo ya Uongozi na Maadili imefunguliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.


Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment