Image
Image

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu na masheikh waungana kukemea uhalifu nchini


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu akitoa hotuba yake katika Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini ya Kiislam katika kuimarisha usalama nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo “Amani na usalama ndio maisha yetu”.
Na Frank Geofray- Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu pamoja na viongozi wa dini ya Kiislamu nchini wameungana kwa pamoja kukemea vitendo vya uhalifu hapa chini pamoja na kuzitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza katika vitendo hivyo.
Rai hiyo ilitolewa leo jijini Dar es salaam na IGP Ernest Mangu pamoja na Viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu katika muendelezo wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini hiyo katika kuimarisha usalama nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo “Amani na usalama ndio maisha yetu”.Mafunzo ambayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu hapa nchini.
IGP Mangu alisema Viongozi wa dini wanadhamana kubwa katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa nchini kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu pamoja na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Alisema wahalifu wa sasa wana mbinu nyingi hivyo kitu kikubwa kitakachoweza kusaidia katika mapambano hayo ni mshikamano wa dhati kutoka kwa viongozi hao katika kuwafichua ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania katika kikao hicho ambaye ni Mjumbe wa Baraza kuu la ulamaa BAKWATA, Sheikh Abubakar Zuber alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani ambazo zimeanza kujitokeza hapa nchini.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia zao na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kubaki salama kwakuwa amani tuliyo nayo ni neema ambayo tunapaswa kuilinda kwa nguvu kubwa.
“Vilevile hatuna budi kuimarisha malezi katika familia zetu mana tunaposhindwa kuwalea watoto wetu vizuri ndio chimbuko la kushamiri kwa vitendo vya uhalifu wa aina mbalimbali hivyo tujielekeze katika kutoa mafunzo bora katika familia”Alisema Sheikh Zuber.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Sheikh Khamis Mataka alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yeyote na hata ndani ya msikiti hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu walio ndani ya misikiti.
Akizungumzia mafunzo hayo Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyibaraka Sheikh Issa Othman alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo viongozi wa dini waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment