Image
Image

Pinda: Watanzania waishio ughaibuni hawatapiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura wakiwa nje ya nchi wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Alisema pamoja na kwamba Watanzania hao wanatakiwa kupiga kura wakati wa uchaguzi huo, jambo hilo halitawezekana kwa sababu kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya uchaguzi huo.
Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo jana kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe, wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio nchini humo.
Akizungumza na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na Manchester, alisema mambo makuu ambayo yanahitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi namba moja ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Najua suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia, kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria na hili zoezi la uandikishaji wa wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Ili mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe ameandikishwa kwenye daftari hilo.
“Itabidi tuangalie kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila ubalozi ili watu wetu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya kufanikisha hilo jambo… lakini watu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye aliwapatia Watanzania hao nakala zisizopungua 40 za Katiba Inayopendekezwa, alitumia fursa hiyo kuwasisitiza waisome kwa makini ili wawe na uelewa mpana na kisha wailinganishe na Katiba ya mwaka 1977 ambayo inatumika hivi sasa ili waweze kubaini kama kweli haina kitu kama ambavyo watu wengine wanadai.
“Moja ya changamoto zinazotukabili huko nyumbani ni mjadala kuhusu Katiba Inayopendekezwa… wako watu wanaosema kwamba hakuna kitu kipya kabisa kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini mimi nasema hayo ni mawazo yao binafsi,” alisema Pinda.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment