Licha ya wizi wa vifaa, kumekuwa na wizi mkubwa wa
magari Dar es Salaam kiasi kwamba mwaka 2013, magari yaliyoibwa ni 400.
Mwaka 2014 yaliibwa 375 na kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu
magari 70 yameibwa.
Kutokana na hali hiyo, polisi jijini Dar es Salaam
wamelaumiwa kwa kushindwa kutokomeza mtandao huo, licha ya wahusika
kufahamika kwa majina, makazi na mahali wanakohifadhi vifaa hivyo vya
wizi.
Hata hivyo, polisi nao kwa upande mwingine
wametupa lawama kwa wananchi wanaoibiwa vifaa hivyo, kuwa hawatoi
ushirikiano kwa jeshi hilo badala yake wameona njia rahisi ni kwenda
kununua upya mali zao kwa wezi hao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya
wananchi walioibiwa vifaa hivyo wanakataa kutoa taarifa polisi kwa
kuhofia kupoteza muda, gari kubaki polisi kama kielelezo hadi vifaa
vipatikane, kutakiwa kutoa fedha kwa wapelelezi au kuhisi kuwa baadhi ya
askari wanahusika na mtandao huo.
Baadhi ya wakazi wa jiji waliowahi kuibiwa vifaa
hivyo wamesema haichukui muda mrefu kwa mtu kubaini mahali vilipo na
kuvipata tena, lakini kwa polisi wenye kila ujuzi kiupelelezi
limeendelea kuwa tatizo.
Vifaa vinavyoibwa zaidi
Kutokana na uchunguzi wa gazeti hili, vifaa
vinavyohitajika zaidi kwa sasa ni side mirror, control box, power
window, vioo vya mbele na nyuma, taa, dash board, redio na baadhi ya
vifaa vya injini.
Magari ambayo vifaa vyake vinaibwa zaidi ni yale
yanayopatikana kwa wingi hasa aina ya Toyota na Suzuki, yakiwamo Escudo,
Altezza, Mark II Grand, Cresta, Verossa, Noah, Ipsum, Klugger, Harrier,
Vitz na Ist ambayo kutokana na wingi wake vifaa hivyo hupata wateja
haraka.
Katika uchunguzi huo Mwananchi limebaini kuwa,
watu wanaoharibikiwa magari, kugongwa au kuibiwa vifaa kwa siku ni wengi
kwa hivyo wezi hupata uhakika wa kuuza vifaa hivyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Upelelezi, Kanda ya Dar es Salaam,
Constantine Massawe alipoulizwa sababu za kukithiri kwa tatizo hilo,
alisema wizi wa vifaa vya magari unashughulikiwa kama uhalifu mwingine,
lakini jeshi hilo halipati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi
wanaoibiwa vifaa hivyo.
0 comments:
Post a Comment