Image
Image

Kiafya juice ya Rosella husaidia mambo mengi mwilini yafahamu hapa.

WATU wengi duniani wamekuwa wakitumia dawa za mitishamba kutibu maradhi mbalimbali, lakini siku za karibu utafiti wa sayansi unaonyesha kuwa mti wa ‘hibiscus sabdarifa’, unaojulikana kama Rosella umeibua habari mpya kuwa unaweza kutibu shinikizo la damu.
Ukizungumza na watu wa makabila, rangi na mataifa mbalimbali, wanasema ukitumia dawa za mitishamba, unaweza kupata nafuu kwa ugonjwa huo. Dawa za mitishamba hiyo si maarufu Afrika pekee, kwa sababu ni maarufu zaidi kwenye vituo vya awali vya afya katika nchi za Ulaya kama Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi.
Umaarufu wa vituo vya kutoa huduma za afya, unaonyesha namna dawa za mitishamba zinavyokubalika na zinavyotumika katika viwanda vingi vikiwamo vya vipodozi. Ukweli kuwa dawa hizo zinatumika, kumebainika pia kwa kuongeza gharama za matumizi ya kila siku katika kutunza afya zao na kuboresha maisha yao.
Miongoni mwa vipodozi vinavyotokana na mitishamba ambavyo vinapendwa na watumiaji wengi ni vile vinavyotumika katika kutengeneza upya ngozi, kuondoa magamba mwilini na kutumika kama krimu ya kulainisha na kuboresha ngozi mwilini.
Duniani, dawa za mitishamba zinatumika zaidi China, India, Japan, Pakistan, Sri Lanka na Thailand. Nchini China, zaidi ya asilimia 40 ya matumizi ya dawa nchini humo ni ya mitishamba. Watu wengi wanaoishi mijini hawana habari juu ya utajiri wa maua na mimea inayowazunguka ambayo Mungu amewapa na ambayo ina faida kubwa katika maisha yao ya kila siku.
Wanasayansi wanathibitisha kuwa mmea wa rosella, unaopatikana katika maeneo mengi nchini, ni tiba muhimu ya shinikizo la damu kuanzia hatua za mwanzo hadi linapofikia hatua ya kati. Hadi sasa majaribio mengi yamefanyika kwa kutibu wanyama na binadamu na yameonyesha mafanikio makubwa upande wa utunzaji na upunguzaji shinikizo la damu. Maji ya miti hiyo yakikamuliwa yanakuwa na ubora sawa na dawa nyingine za hospitalini zinazotibu shinikizo la damu.
Mfumo wa namna ya kutengeneza dawa za kushusha kiwango cha shinikizo la damu bado unahitaji kufanyiwa utafiti zaidi. Lakini matokeo yaliyopatikana kutokana na kutibu wanyama, yameonyesha wazi kuwa mmea huo unatoa tiba salama na haujasababisha madhara kwa wanyama na binadamu.
Pamoja na kupunguza shinikizo la damu, utengenezaji dawa kutokana na mti huo pamoja na vikonyo vya majani yanayohifadhi maua ambayo kabla hayajachanua yanasaidia kupunguza mgandamizo wa damu mwilini.
Dawa hiyo ina kazi ya kupunguza oksijeni mwilini na inaweza pia kutumika kuzuia kansa na magonjwa kwenye maini, hasa kwa wanywaji wa pombe. Ni nzuri kuitumia kwa wagonjwa wa upungufu wa damu kwani imeonyesha wazi ina uwezo wa kuimarisha nyumba zinamokaa chembechembe nyekundu za damu.
Dawa hiyo inasaidia kuhuisha upya maisha ya mtu mwenye upungufu wa damu. Kwa upande wa chakula bora, dawa hiyo ni tajiri wa vitamani C, thiamin, riboflavin na niacin. Pia ina madini muhimu mwilini ambayo ni calcium, phosphorus na chuma.
Kwa miaka mingi, rosella imekuwa ikitumika katika nchi mbalimbali kama nishati muhimu ya kupikia na chanzo mahususi cha dawa za kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu. Dawa hii ilitumika kwa wingi barani Asia, Amerika Kusini, Visiwa vya Caribbeani, Ulaya na Asia. Ilitumika katika kuandaa mishumaa, mafuta na viungo moto na baridi na ilitengeneza mvinyo mzuri wa kunywa.
Ukichanganya na chai utajisikia unakunywa kinywaji chenye harufu nzuri inayonukia kama dawa na kama kirutubisho mwilini. Si ajabu kusikia dawa hiyo baada ya kunywa inaondoa uchovu, mafua na maradhi ya tumbo hasa ya kujaa gesi.
Taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inasema, ‘kuzuia magonjwa sumbufu, ni uwekezaji muhimu.’ changamoto iliyopo kwa taasisi za magonjwa ya moyo na kupooza, miongoni mwa taasisi nyingine, ni kutakiwa kuponya maisha ya watu milioni 36 duniani ambao wanaweza kuwa wamekufa kufikia mwaka 2015.
Kuwa dawa hiyo inatibu shinikizo la damu ni faraja kwetu sote, kwa sababu magonjwa ya mifumo ya hewa imetokea kuwa miongoni mwa magonjwa sugu yanayosumbua afya ya jamii katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.
Kwa mujibu wa Profesa Jacob Mtabaji, katika Tanzania, magonjwa ya mifumo ya hewa yanachangia asilimia 15 ya vifo vya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 30, na hivyo kuufanya ugonjwa huo kusababisha vifo vingi kwenye kundi hilo.
Hivi karibuni utafiti umeonyesha kuwa asilimia sita ya vifo hivyo nchini Tanzania vinatokana na kupooza kwa watu wazima wenye umri kati ya miaka 15 na 64. “Vifo vya kupooza kwa mwaka ni watu 65 kati ya watu 100,000 kwa wanaume, wakati wanawake ni 88 kati ya 100,000, kumbe Uingereza na Wales ni 10.8 kwa wanaume na wanawake ni 8.6,” anasema Profesa Mtabaji.
Idadi ya vifo vya kupooza katika Tanzania vinatokana na kutotibiwa kwa wagonjwa wengi wanaopata maradhi ya shinikizo la damu. Jijini Dar es Salaam, utafiti unaonyesha kuwa watu wengi wanaoathirika na ugonjwa huo ni wenye umri mkubwa. Kwani asilimia 21.8 ya wanaume wenye umri wa miaka 50-54 wana shinikizo la damu, wakati asilimia 30.9 ya wanawake wenye umri wa miaka 50-54 ndiyo wenye ugonjwa huo.
Kundi la watu wenye umri wa miaka 40 hadi 44, kiwango cha shinikizo la damu kwa wanaume ni asilimia 6.4 na wanawake 11.5. Wakati kundi la watu wenye umri wa miaka 30 hadi 34, kiwango cha shinikio la damu ni asilimia 6.4 wanaume na wanawake ni asilimia 5.9. Maendeleo ya utafiti wa miti ya habiscus sabdariff umekuja wakati muafaka ambako dawa za mitishamba zinapata umaarufu nchini mwetu kutokana na juhudi za watafiti mbalimbali walioamua kuinua kiwango cha dawa za mitishamba nchini.
Mti huo unapatikana Tanzania na unapandwa mkoani Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma na Pwani. Taasisi ya Dawa za Mitishamba katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUCHS), inaitambulisha dawa hiyo kama chanzo cha kuleta lishe bora na kinywaji chenye kuleta afya.
Kinachotakiwa ni kuchukua maganda ya miti hiyo na kuchanganya na maji, halafu tikisa na utapata kinywaji kizuri cha kuburudisha. Mti huu ni miongoni mwa mimea ambayo ipo kwenye mradi wa kutaka liwe zao la kuzalishwa katika maeneo mengi ili liwe chanzo cha mapato kwa wakazi wa Kongowe, mkoani Pwani.
“Mpango wa muda mrefu wa zao hilo ni kupanga daraja la uwezo wa zao, ama kutibu peke yake au kwa kuunganisha na dawa nyingine,” anasema Dk. Mainen Moshi, kiongozi wa mradi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mitishamba, Muhimbili. Mradi huo una malengo mawili, kwanza, una lengo la kuchangia katika mkakati wa kitaifa wa kupunguza umaskini kwa kuzalisha zao hilo na kuwa chanzo cha lishe bora na kuongeza kipato cha wananchi.
Pili, ni kuchangia katika uboreshaji sera za taifa za chakula na lishe bora ambazo zinalenga katika kuongeza mazingira ya uzalishaji lishe bora miongoni mwa watoto na wanawake hata wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Kuwapo kwa mmea huo nchini, ni kitu kizuri na cha kujivunia, na hivi karibuni, wanasayansi wamekuwa wakiutangaza kwa nguvu zao zote, kuhakikisha taifa linatambua umuhimu wa mti huo na namna linavyoweza kuutumia.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment