Image
Image

Korea Kusini na Kaskazini zakubaliana kufanya mazungumzo.

Korea Kusini na Korea Kaskazini zimekubaliana kuhudhuria mazungumzo ya maafisa wa ngazi za juu, kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili na kuondoa mvutano uliopo baina yao. 
Mazungumzo hayo yatakayofanyika tarehe 26 ya mwezi huu wa Novemba yatakayokuwa ya aina yake, ni ya kwanza kufanyika tangu maafisa wa Korea Kusini na Korea Kaskazini walipokutana mwezi Agosti mwaka huu, kwa lengo la kuzuia mgogoro ambao bado kidogo usababishe nchi hizo mbili kuingia katika mzozo wa kivita.
Wizara ya Muungano ya Korea Kusini imesema leo kuwa imeupokea mwaliko uliotolewa na Korea Kaskazini wa kushiriki katika mazungumzo hayo yatakayofanyika kwenye kijiji kilichoko mpakani cha Panmunjom. Wizara hiyo imesema mwaliko huo umetolewa na kamati ya Korea Kaskazini inayoshughulikia amani ya kuungana kwa Korea.
Kulingana na makubaliano ya mwezi Agosti, Korea Kusini ilizima vipaza sauti vyake vilivyokuwa vinatangaza ujumbe wa propaganda katika eneo la mpakani, baada ya Korea Kaskazini kuelezea kusikitishwa kwake na milipuko miwili ya mabomu ya hivi karibuni ya kutegwa ardhini ambayo iliwajeruhi wajeshi wawili wa Korea Kusini.
Korea Kusini iliilaumu Korea Kaskazini kuhusika na milipuko hiyo, shutuma ambazo ilizikanusha, ikisema haihusiki. Hata hivyo, Korea Kusini iliyachukulia matamshi ya Korea Kaskazini kama ''kuomba radhi'', lakini tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa ikisisitiza kwamba kauli yake ilimaanisha huruma pekee.
Uhusiano mbaya
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa mbaya hadi kufikia ule wa baada ya vita kutokana na kuzama kwa meli ya kivita ya Korea Kusini mwaka 2010, tukio jingine ambalo Korea Kusini imeilaumu jirani yake kwa kuhusika.
Kulingana na makubaliano ya mwezi Agosti, mataifa hayo yalifanikiwa kuziunganisha familia zilizotenganishwa na vita ya Korea vya mwaka 1950 hadi 1953 na hivyo kusababisha nchi hiyo kujitenga. Zoezi hilo lilifanyika mwezi uliopita wa Oktoba. Nchi hizo mbili zimeshawahi kufanya mikutano miwili ya kilele, ambapo mmoja ulifanyika mwaka 2000 na mwingine mwaka 2007.
Korea Kaskazini pia inakabiliwa na vikwazo kadhaa kutoka kwa Umoja wa Mataifa, vilivyowekwa baada ya nchi hiyo kufanya majaribio matatu ya silaha za nyuklia mwaka 2006, 2009 na 2013.
Katika hatua nyingine, siku ya Jumatatu Umoja wa Mataifa ulikanusha taarifa kwamba Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-Moon anapanga kuzuru Korea Kaskazini wiki hii, ingawa umoja huo unafahamu uko katika mazungumzo na nchi hiyo kuhusu ziara ya Ban Korea Kaskazini ikiwezakana kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mwezi Mei mwaka huu, Ban alipangiwa kuzuru Korea Kaskazini, lakini nchi hiyo iliufutilia mbali mwaliko huo dakika za mwisho, baada ya kiongozi huyo kuikosoa Korea Kaskazini kutokana na jaribio lake la kombora hivi karibuni.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment