Image
Image

Sadiki:Zoezi la usafi siku ya sherehe za uhuru ni Endelevu

Na Lilian Lundo-MAELEZO
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa  mazingira litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara  tarehe 9 Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata  baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo.
Mhe. Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano. Mhe. Dkt John Pombe Joseph  Magufuli aliagiza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara  mwaka huu yatumike kwa kufanya usafi wa Mazingira kote nchini badala ya  kufanya sherehe za gwaride la askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Akiongea na vyombo vya habari leo Mhe. Sadiki alianza kwa kumpongeza Mhe. Rais
kwa uamuzi aliouchukua wa kubadilisha sherehe za uhuru kuwa ni siku ya  kufanya kazi badala ya kwenda uwanjani na kuangalia gwaride na halaiki  mbalimbali kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita. 

“Mhe.Rais katurejesha kule tulipotoka ambako kauli mbiu ya sherehe za uhuru ilikuwa ni uhuru na kazi au uhuru ni kazi wakati watanzania walikuwa  wakiungana na kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana,” alisema, Mhe. Sadiki.
Aidha, Mhe Sadiki alisema, zoezi la usafi kwa mkoa wa  Dar es Salaam litaanza rasmi tarehe 1 Disemba mwaka huu na kumalizikia 9 Disemba mwaka huu siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru na  kuongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.
Mhe. Sadiki  aliongeza kwa kusema kuwa, uongozi wa mkoa umewaomba wadau kujitokeza
kwa kuchangia fedha au vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na  amewataka watendaji kushawishi wananchi wa maeneo yao kutafuta vifaa  badala ya kusubiri kuletewa na Halmashauri.
Pia, Mhe Sadiki  amewahimiza watendaji wa mitaa na kata kutimiza wajibu wao wa
kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi muda  wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko na pale inakapobainika eneo  fulani lipo katika mazingira ya uchafu basi mtendaji wa eneo hilo  atawajibishwa kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kosa la
kutotimiza wajibu wake.
Vilevile ametoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi kwa kuacha tabia  za kutupa taka ovyo hasa wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na  kutokujisaidia katika mitaro au vichaka ili kuepukana na uchafuzi wa  mazingira kunakopelekea kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment