Image
Image

BASATA yamfungia Ney wa Mitego kutojihusisha na muziki kwa muda usiojulikana.


Leo 27 Julai 2017 Mkali wa Muziki wa Hip hop nchini Tanzania anaye tambulika kwa tungo zake zenye ukakasi na zisizoficha jambo, Ney wa Mitego amefungiwa kujihusisha na sanaa ya muziki kwa kipindi kisichojulikana kufuatia wimbo wake alioutoa hivi karibuni unaitwa ‘Pale kati patamu’.Wimbo huo ambao tarehe 18 Julai 2017 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitangaza kuufungia rasmi kwa kile ilichokisema kuwa ni kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza siku ya 18 Julai 2017, ilieleza kuwa msanii huyo amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua sekta ya sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonyesho yenye kukiuka maadili.
“Kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.”Alisema Mngereza
Mngereza alisisitiza kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.
“Ikumbukwe kwamba BASATA limeshamuita na kumuonya msanii huyu mara kadhaa kutokana na tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo. 
Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. Kwa sasa Msanii huyu ametoa wimbo mwingine wa Pale Katipatamu ambao uko mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama.”
Aidha Katibu Mtendaji huyo wa Basata, Godfrey Mngereza amesema licha ya adhabu hiyo Ney anatakiwa pia kulipa faini ya Sh1 milioni.
------------------------------------------------------------------------------
 Nay wa Mitego afungiwa kujihusisha na muziki kwa muda usiojulikana na Faini ya shilingi milioni 1.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego hadi hapo litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na Baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo dhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Maagizo aliyopewa Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha Shilingi milioni 1, kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya Sanaa kwa maana ya kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.
Aidha, Msanii Nay ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususan wanawake.
Maamuzi haya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Adhabu hizi zimetolewa kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu jana siku ya Jumanne tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye kukiri makosa na kuahidi kubadilika.
Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;

1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.
2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.
3. Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.
Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yenye uvunjifu mkubwa wa maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha, tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako wa Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya. Hivyo adhabu hii imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama kweli ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment