Fredrick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye,
amewashukia ‘vigogo’ wenye madaraka, kuwa wanahusika kushamirisha biashara ya
dawa za kulevya, wakiwatumia vijana katika kufikia malengo yao.
Sumaye amesema, mbali na ‘vigogo’ hao, biashara
hiyo inawahusisha baadhi ya wafanyabiashara wenye nguvu kubwa za kiuchumi, na
kusisitiza hakuna sababu kwa jamii kuogopa ama kulifumbia macho tatizo hilo.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni kiongozi pekee
aliyehudumu wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa muda mrefu (miaka 10), hakuwataja kwa
majina vigogo ama wafanyabiashara hao.
Lakini katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo
taarifa zinazowahusisha baadhi ya wanasiasa, akiwamo Mbunge wa Kinondoni, Idd
Azzan (CCM) ambaye hata hivyo, alikana kuhusika katika biashara hiyo.
Pia, aliyewahi kuwa Mbunge kupitia Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, aliwahi kutamka
kuhusu kuwapo viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara wanaojishughulisha na
biashara hiyo, akitaka serikali iwashughulikie.
“Hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulifumbia
macho. Biashara ya dawa za kulevya inafanywa na watu wazito ama kwa fedha zao
au kwa madaraka yao,” alisema Sumaye.
Sumaye alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa
Kituo cha Maendeleo ya vijana (Tayodec) mjini Arusha jana.
Alisema hivi sasa nchi inaonekana kuwa kituo
muhimu cha kupitishia dawa hizo kwenda ama kutoka katika mataifa mengine.
“Hii siyo sifa nzuri kwa nchi yetu. Lakini
ukiachilia mbali madhara ya kupitishia nchini, dawa hizo zinawathiri sana
vijana wetu na kuwageuza mazezeta kwa baadhi ya wale wanaozitumia,” alisema.
Kwa mujibu wa Sumaye, uhalifu mwingi wa kutisha
unafanywa na watu wanaozitumia dawa hizo, huku vijana wanatumika kuzibeba
kwenye miili yao, hali inayohatarisha maisha yao ikiwamo kufa.
“Cha kusikitisha wenye biashara hiyo wao
hawaendi kuleta hizo dawa wala hawawatumii watoto wao, bali watoto wa wenzao
ili wakikamatwa na vyombo vya dola au kudhurika kwa ubebaji huo, iwe ni shauri
yao,” alisema.
“Hii ni roho mbaya tena ya kinyama sana, kuona
wewe kupata fedha hizo chafu kwa gharama ya mtoto wa mtu mwingine, ati ni sawa
tu. Lazima tujali watoto wa wenzetu kama watoto wetu,” aliongeza.
ASEMA ANAHUJUMIWA KWA VIJANA
Sumaye alisema Tayodec ni taasisi
inayoshughulika na vijana, ikimteua kuwa mlezi wake, lakini akipata upinzani
kutoka kwa watu wasiomtakia mema.
Alisema watu hao (hakuwataja majina), wameiona
taasisi hiyo kama mtaji wa kisiasa na kutaka kuitumia kwa malengo hayo.
“Najua mmeshawishiwa kwa ahadi ya fedha nyingi
na wakati huo huo kunikejeli mimi kuwa sina fedha. Nadhani hawakujua kuwa moja
ya malengo makuu ya taasisi ni kupiga vita rushwa na tabia ya kununua watu na
mngekubali kununuliwa basi ndiyo ungekuwa mwisho wa taasisi yenu,” alisema.
WAWILI WASIMAMISHWA JNIA
Wakati Sumaye akitoa angalizo hilo, maofisa
wawili wa kitengo cha ukaguzi katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA)
jijini Dar es Salaam, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi unaohusishwa na
kukamatwa kwa dawa za kulevya nchini Afrika Kusini.
Hivi karibuni, wasichana wawili wa Tanzania,
Agnes Jerald (25) maarufu kama Masogange na Melisa Edward (24), walikamatwa
nchini humo wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, zenye
thamani ya Sh. bilioni 6.8, zikitokea hapa nchini.
Washitakiwa hao ambao walikatwa katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo jijini Johannesburg, wakiwa na kilo
150 za dawa hizo zilizohifadhiwa kwenye masanduku sita.
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Poul Rwegasha,
aliimbia NIPASHE Jumapili kuwa kufuatia sakata la dawa hizo, wamewasimamisha
kazi maofisa hao ambao hakuwataja majina wala taasisi wanazofanyia kazi, ili
kupisha uchunguzi.
“Siku ya tukio hilo, tuliangalia kamera za
usalama (CCTV) na kuwaona maofisa hao, hivyo tumewasimamisha kwa ajili ya
uchunguzi na siyo kwamba wamefukuzwa kazi,” alisema.
Alisema kwa hatua hiyo, wameondolewa kwenye kitengo
cha ukaguzi, ingawa bado wanafika kazini wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea.
Kwa mujibu wa Rwegasha, maofisa wawili wa
polisi, ni miongoni mwa walioonekana kwenye CCTV hiyo, ingawa hakutaja majina
yao.
Alisema hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu
kuhusika kwa askari hao, hivyo uchunguzi ukikamilika hatua zinazostahili
zitachukuliwa.
“Siyo vizuri kukutajia majina ya hao maofisa
kwani utaharibu uchunguzi wetu, na bado hawajakutwa na hatia, uchunguzi
utakapokamilika nitakupatia taarifa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Deusdedit
Kato, alisema zaidi ya watu 10 wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo, na kwamba
watajulikana pindi uchunguzi utakapokamili.
Chanzo Nipashe.
0 comments:
Post a Comment