Zaidi ya wakazi 200 waliookolewa katika maeneo yao katika
mitaa ya Madale, Boko na Mabwepande Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,
wameanza kutambuana wenyewe kwa wenyewe kabla ya manispaa haijaanza zoezi la
upimaji ardhi hivi karibuni.
Akizungumza na Tambarare Halisi, Mwenyekiti wa kamati ya wakazi hao, Pascal
Lutege, alisema walikuwa na zoezi la uhakiki wa kufahamiana wenyewe katika
mipaka.
“Tumekutana ili kila mtu aweze kumfahamu jirani
yake katika pande zote, kwani Manispaa ya Kinondoni imesisitiza itaanza zoezi
la kuwaondoa wavamizi waliosalia wiki ijayo…tukijuana wenyewe itakuwa ni rahisi
kwa manispaa kuendelea na zoezi lao,” alisema Lutege.
Lutege alifafanua kwa kusema maeneo yanayohusika
na zoezi hilo la utambuzi ni yale ambayo yaliokolewa na serikali toka mikononi
mwa wavamizi wa ardhi huko Nakalekwa (Boko), Nakasangwe, Kazaroho (Madale)
pamoja na Kinondoni iliyopo mtaa wa Mabwepande.
Alisema baada ya uhakiki huo uliofanyika jana,
watasubiri tamko la manispaa ya kwenda eneo la mashamba na kila mmiliki
atakuwapo na hati zake kwa ajili ya utambuzi.
“Tumejiandaa hivi baada ya Meya wa Manispaa,
Yusuph Mwenda kuweka saini katika mikataba yetu na manispaa yake kwa ajili ya
zoezi la upimaji kwa kuendeleza maeneo hayo ambayo wamiliki wamekubali kuachia
asilimia 40,” alisema.
Hata hivyo, Meya Mwenda amewasisitizia watu
wanaoendelea kujenga katika maeneo ambayo yalikombolewa na serikali, kuondoka
mara moja ili kupisha zoezi la upimaji kufanyika kirahisi na hatasita kutumia
nguvu kuwaondoa.
0 comments:
Post a Comment