Zaidi ya watoto 600 wakimbizi kutoka Burundi
wamepotezana na wazazi wao katika harakati za kukimbia nchi yao au kuhamishwa
kutoka kambi moja kwenda nyingine mkoani Kigoma.
Baadhi ya watoto hao, walipotezana na wazazi wao
wakati wa kupanda meli za Mv Liemba na Mv Malagarasi kutokea Burundi na wengine
katika harakati za kwenda Kambi ya Nyarugusu.
Toka Mei Mosi, mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linawasafirisha wakimbizi hao kutoka kambi moja
hadi nyingine kwa kutumia meli za Mv Liemba na Mv Malagarasi. Hata hivyo,
kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi katika kambi zote pamoja na utaratibu
mbovu wa kuwahamisha kutoka kambi moja kwenda nyingine.
Mfanyakazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa
(IOM), Frederick Moses alisema uhamishaji ulikuwa haufuati utaratibu maalumu
kwa kuwa meli moja kutoka Kagunga kwenda mjini Kigoma ilikuwa inabeba wanaume
tu au wanawake tu na nyingine watoto pekee hali iliyosababisha familia
kupotezana.
Takwimu kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii iliyopo
katika kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika, zinaonyesha kuwa Mei 18, mwaka huu,
watoto 53 walipotea, Mei 19 walipotea 124, Mei 20 (160), Mei 21 (81), Mei 22
watoto 145 na Mei 24 walipotea watoto zaidi ya 20.
Hata hivyo, Mollel alisema Ustawi wa Jamii kwa
kushirikiana na Shirika la Plan International, Unicef na Kamati ya Uokoaji ya
Kimataifa (IRC), wanafanya kazi ya kuwatambua watoto waliopotea au waliotengana
na wazazi wao na kuwatafutia wazazi wa muda wa kuwalea.
Msemaji wa Plan International, Emmanuel Kihaule
alisema watoto hao huhifadhiwa hadi pale wazazi wao watakapopatikana na wale
wagonjwa huwekwa katika uangalizi maalumu wa tiba.
“Wapo pia walioathirika kisaikolojia kutokana na
kufanyiwa ukatili wa kijinsia, wako kwenye uangalizi maalumu,” alisema.
Baadhi ya watoto hao walisema waliondoka Burundi
peke yao huku wengine wakisema walikuwa wanaishi mitaani mjini Bujumbura na
waliposikia mapigano wakaamua kufuata mkumbo wa kukimbia.


0 comments:
Post a Comment