WATU watano ambao ni wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Nyangalata
wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, wameokolewa na wenzao baada ya
kufukiwa na kifusi cha udongo na kukaa kwa muda wa siku 41.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakiwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Kahama walipolazwa, wachimbaji hao walisema walikuwa katika shimo
hilo kwa siku hizo huku wakila wadudu, hususan mende, pamoja na mizizi
ya miti. Halikadhalika wanasema walitumia kofia zao kukinga maji
yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi na kunywa.
Mmoja wa wachimbaji hao, Chacha Wambura, alisema katika shimo hilo,
walifukiwa sita, lakini mwenzao, Musa Spana alifariki dunia baada ya
kukataa kula mizizi na kisha kupata ugonjwa wa kuhara uliosababisha kifo
chake. “Tulikuwa tukitumia miti inayojengea mashimo (matimba) kama
chakula sambamba na wadudu wadogowadogo na maji tulikuwa tukitumia kofia
zetu kukinga maji yaliyokuwa yakitoka juu ingawa yalikuwa ni machafu.
Mwenzetu mmoja, Musa Spana alifariki dunia baada ya kukataa kutumia
vitu hivyo,” alisema Wambura. Kwa mujibu wa mchimbaji huyo, waliokolewa
baada ya wachimbaji wenzao waliokuwa jirani na shimo ambalo walitumbukia
ambapo walipokuwa wakifanya kazi hiyo ya uchimbaji na kufika chini,
wakasikia sauti za watu. Alisema shimo lao lilikuwa umbali wa meta 200
kutoka ardhini, hivyo wachimbaji wenzao walipofika chini jirani na shimo
lao, walisikia sauti zao, wakarudi juu na kuwaarifu wananchi wengine.
Kwa mujibu wa Wambura, baadaye wachimbaji hao kwa kushirikiana na
wananchi walianza jitihada za kuwaokoa na kufanikiwa kuifanya kazi hiyo
juzi, lakini maiti ya mwenzao Spana haijaopolewa. Naye Naibu Kamishna wa
Madini nchini, Ali Samaje aliwataka wachimbaji wadogo kuimarisha migodi
huku wakizingatia masuala ya kiusalama zaidi, hali itakayowawezesha
kufanya kazi zao kwa uhakika na kuepuka ajali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Joseph Ngowi,
alisema ameshtushwa na tukio hilo la wachimbaji kukaa kwa muda huo
shimoni, na kuongeza kuwa tukio hilo linaweza kuwa ni maajabu ya nane ya
dunia.
Alisema waathirika hao wapo katika hospitali hiyo chini ya usimamizi
wa Kitengo cha Lishe na Saikolojia ili kuhakikisha kuwa wanarudi katika
hali zao za kawaida kwa muda usiopungua siku saba.
“Hawa jamaa tunao katika hospitali yetu, na hawaoni kwa muda huu
mpaka muda wa siku saba upite, kwani sehemu waliyokuwepo palikuwa ni
giza, hali ambayo kwa sasa bado macho yao sio mazuri pamoja na akili zao
sio nzuri,” alifafanua.
Pia alisema kutokana na kukaa shimoni kwa muda mrefu, hali zao ni
dhaifu na utumbo bado haujawa vizuri kwa hiyo kwa kuwatumia wataalamu wa
Idara ya Lishe kwa sasa wanawatengenezea chakula laini kama vile uji
ili wapate nguvu, na wanatarajia ndani ya siku saba hali zao zitaanza
kutengamaa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha akizungumza kwa
simu alikiri kutokea kwa ajali hiyo katika mgodi wa wachimbaji wadogo
wa Nyangalata na kuongeza wanaendelea na uchunguzi.
Akizungumza mjini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa Wizara ya Nishati
na Madini, Badra Masoud aliwataka wachimbaji wadogo kuhakikisha
wanatumia vifaa vya kisasa ili kuepusha matatizo kama haya.
Badra alisema ni lazima wachimbaji hao wawe makini katika suala zima
la uchimbaji kwa kuhakikisha wanatumia vifaa vya kisasa ili
kujihakikishia usalama wao. “Wengi wanachimba tu bila kuwa na vifaa
vyenye uhakika linapotokea tatizo kama hili inakuwa ngumu kukabiliana
nalo ni vyema wakatumia vifaa salama ambavyo vitawahakikishia usalama
wao,” alisema. Alisema wizara hiyo inaendelea na juhudi zake ili
wafanikishe kuupata mwili wa Supana ambao upo katika machimbo hayo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment