Waziri Mkuu wa Uingereza David
Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamekutana karibu na jiji la
Berlin siku ya Ijumaa, kama sehemu ya juhudi za Uingereza kushinikiza kuwepo
mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya.
Merkel alimualika Cameron na mke wake Samantha,
na watoto wao watatu katika kasri la wageni la serikali ya Ujerumani la
Meseburg, lililoko umbali wa kilomita 70 kusini-magharibi mwa Berlin.
Mazungumzo ya siri kati ya Merkel na Cameron yalipangwa kufanyika Ijumaa jioni
na Jumamosi asubuhi. Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert alisema kabla
ya mazungumzo hayo siku ya Ijumaa, kuwa Uingereza ni mshirika muhimu sana kwa
Ujerumani katika Umoja wa Ulaya.
Cameron na Merkel |
Cameron ambaye chama chake cha kihafidhina kina
kundi lenye nguvu linalopinga uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya,
anafanya ziara kwa viongozi wa Ulaya, katika jitihada zake za kushinikiza
mabadiliko ndani ya Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na kuzipatia nchi wanachama
haki ya kujitenga na baadhi ya sheria za umoja huo. Wiki hii alikatisha ziara
fupi mjini Madrid Uhispania, na alikuwa akipanga upya mazungumzo na rais wa
Ufaransa, Francois Hollande, baada ya kifo cha waziri mkuu wa zamani, Margaret
Thatcher
Waziri mkuu wa Uingereza David
Cameron akijiandaa kusaini kitabu cha wageni, akishudiwa na mwenyeji wake
Kansela Merkel, mke wake Samantha, na mume wa Merkel Joachim Sauer.
|
Cameron alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa
Ujerumani na Ufaransa mwaka huu, alipotangaza mipango ya kujadili makubaliano
mapya kwa Uingereza, na baadae kuendesha kura ya maoni kuhusu uanachama wa
Uingereza kufikia mwaka 2017. Cameron alinukuliwa wiki hii akisema kuwa Ulaya
itakuwa yenye mafanikio zaidi kama itakuwa na nguvu ya mabadiliko, kuliko
udhaifu wa kutotaka mabadiliko. "Nadhani matokeo mazuri zaidi kwa
Uingereza ni uanachama wetu wa Umoja wa Ulaya uliyofanyiwa mabadiliko,"
alisema waziri mkuu Cameron.
Ajenda nyingine za mkutano wao
Merkel na Cameron pia walipanga kujadili mpango
wa nyuklia wa Iran, vita vya nchini Syria, na mkutano mkuu wa kilele wa Kundi
la mataifa manane, utakaofanyika mwezi Juni katika Ireland ya Kaskazini, kwa
mujibu wa msemaji wa Kansela Merkel. Ujerumani pia ilitrajiwa kuishinikiza
Uingereza juu ya haja ya kuchukua hatua kushughulikia mataifa mbalimbali
duniani, ambako baadhi ya kodi hutozwa kwa kiwango kidogo sana au hazitozwi
kabisaa.
Kansela Merkel akimtembeza mgeni wake ndani ya kasri la Meseberg. |
Kwa muda mrefu, wabunge wa Ujerumani wameonyeshwa
kukatishwa kwao tamaa na uhusiano wa Uingereza wa kujitenga na Umoja wa Ulaya,
ukiwemo uamuzi wa Cameron mwaka 2009, kukiondoa chama chake cha kihafidhina
kutoka kundi la nadharia za mrengo wa kati, kuelekea kulia katika bunge la
Ulaya, ambalo linajumuisha pia chama cha Kansela Merkel cha Christian
Democratic Union, CDU.
0 comments:
Post a Comment