Mkoa wa Dar es Salaam- Said Meck Sadick
Ndugu Wananchi wa Mkoa wa
Dar es Salaam,
Napenda
nichukue fursa hii kuwajulisha rasmi kwamba Nchi yetu imepata heshima ya
kutembelewa na Waziri Mkuu wa Thailand ambaye atawasili Nchini tarehe
30/07/2013. Ziara hii ni ya kikazi (state visit) na atawasili katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kumbukumbu ya Mwalimu J. K. Nyerere majira ya
saa 6:30 mchana na kulakiwa na mwenyeji wake Mhe. Rais wetu mpendwa Dr. Jakaya
Mrisho Kikwete akifuatana na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Mkoa.
Ndugu Wananchi,
Baada ya
kuwasili Mhe. Waziri Mkuu wa Thailand atakagua gwaride maalum lililoandaliwa
kwa ajili yake na pia atapata fursa ya kukagua vikundi mbalimbali vya ngoma
ambavyo vitakuwa vikitumbuiza na kutoa burudani kwa Mgeni wetu na msafara wake.
Ndugu Wananchi,
Mgeni wetu
baada ya kukagua vikundi vya ngoma na burudani ataondoka kuelekea Ikulu kupitia
barabara ya Nyerere, Railway, Gerezani, Sokoine Drive hadi Ikulu. Akiwa Ikulu
atasaini mikataba mbalimbali kati ya Serikali ya Tanzania na Thailand. Usiku
atashiriki katika dhifa maalumu iliyoandaliwa na Mwenyeji wake.
Ndugu Wananchi,
Tunaomba radhi
kwamba barabara hizi nilizozitaja zitafungwa kwa muda kupisha misafara ya
Viongozi wetu Wakuu watakaoelekea Uwanja wa Ndege wa Kumbukumbu ya
Mwalimu J. K. Nyerere kumlaki Mgeni wetu hususan barabara ya Nyerere kuanzia
saa 6.00 mchana hadi saa 7.30 mchana.
Ndugu Wananchi,
Tarehe
31/07/2013 Waziri Mkuu wa Thailand atatembelea Mbuga za Wanyama za
Serengeti.Tarehe 01/08/2013 atarejea Dar es Salaam na kuagwa rasmi katika
Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere na kuendelea na ziara yake huko Uganda.
Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada
tunaombwa kumlaki mgeni wetu kwa shangwe na bashasha katika maeneo yote
atakayopita.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Saidi Meck Sadiki
MKUU WA MKOA
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment