Na Bonface Wambura TFF.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake
kimejiandaa kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi
ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa
Jumamosi jijini Kampala.
“Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na
Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo
mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema
Kim.
Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji
kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwa
wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na
kupumzika.
“Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la
kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu
ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na
kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya
beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
inaondoka Mwanza kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya
PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15
mchana.
Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja,
Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto
Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni
Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva.
Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
0 comments:
Post a Comment