Paul Kagame kulia.
ONYO lililotolewa na Ikulu ya Marekani dhidi ya Serikali
ya Rwanda, linalomtaka Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, kuacha kuwasaidia waasi
wa kikundi cha M23, lina kila dalili zinazomuweka kwenye kundi la viongozi wa
Kiafrika ambao hatma yao baada ya kuachia madaraka inazungukwa na wingu la
mashaka.
Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye mapema wiki hii
alikaririwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani akimtaka Rais Kagame kuacha
kukisaidia kijeshi kikundi cha waasi wa M23, anaaminika kuitoa kauli hiyo kama
msimamo wa serikali yake inayopinga watawala wanaojihusisha na uhalifu wa
kivita.
Ingawa hadi sasa Rais Kagame hajatajwa na Ikulu ya
Marekani kama mmoja wa viongozi wa Afrika wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita,
onyo lililotolewa na Rais Obama linadhihirisha kuwepo kwa ushahidi unaomhusisha
na matukio ya aina hiyo yaliyopata kuwagharimu baadhi ya marais walionyooshewa
kidole na Marekani kwa aina hii hii anayonyooshewa sasa Kagame.
Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo walioichambua kauli ya
Rais Obama, wanaeleza kuwa aliitoa baada ya Marekani kujiridhisha na ushahidi
ilioukusanya ukiihusisha Serikali ya Rwanda kuwasaidia waasi wa kundi la M23.
Wanaeleza kuwa Marekani baada ya kubaini ushirika wa
majeshi ya Rwanda yaliyojipenyeza ndani ya makundi ya waasi wanaopigana na
Serikali ya Kongo, huku wakitekeleza vitendo vya kinyama dhidi ya binadamu
katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini,
imeamua kumtosa Kagame, ambaye amekuwa na uswahiba wa muda mrefu na taifa hilo.
Katika tathimini yao kuhusu uzito wa onyo la Rais Obama
kwa Rais Kagame, wanaeleza kuwa hataweza kuepuka kitanzi cha mashitaka katika
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Waasi wa kikundi cha M23, mbali na kuendesha mapambano
dhidi ya majeshi ya Serikali ya Kongo, jambo linalopingwa na jumuiya ya kimataifa,
pia wanatuhumiwa kwa ubakaji na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Tuhuma hizo pia zinaelekezwa kwa majeshi ya Rwanda,
yanayodaiwa kushirikiana na waasi hao na ndizo zinazomuweka Rais Kagame katika
hatari ya kufikishwa mahakamani na hata kuhukumiwa kama ilivyokuwa kwa
aliyekuwa Rais wa Liberia, Charles Taylor, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo
cha miaka 50 jela baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita nchini
Sierra Leone ambako zaidi ya watu 50,000 waliuawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe
na wengine wengi wakiachwa na ulemavu wa kudumu.
Kama inavyotokea kwa Rais Kagame sasa, kwa Taylor pia
ilikuwa hivyo hivyo, pale alipokuwa akionywa na jumuiya za kimataifa na yeye
kudharau maonyo hayo.
Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo
huo kuhusu onyo la Serikali ya Marekani dhidi ya Rais Kagame kujiingiza kijeshi
katika vita vya ndani ya Kongo, ushahidi uliokusanywa na taasisi za Umoja ya
Mataifa za kutoa misaada ya kibinadamu unaonyesha kuwa wanajeshi wa Rwanda
wanaopigana bega kwa bega na waasi wa M23 wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya
kihalifu dhidi ya binadamu.
Ni ushahidi wa aina hiyo ndio uliotumiwa na ICC,
kumhukumu Taylor, aliyekuwa akituhumiwa kuvisaidia vikundi vya waasi vya
Revolutionary United Front (RUF) na Armed Forces Revolutionary Council (AFRC)
kwa kuvigawia silaha za kivita kwa muktadha wa kupewa madini ya almasi.
Stephen Rapp, mchambuzi wa sheria za makosa ya jinai wa
Marekani, katika mahojiano yake na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza,
alieleza kuwa uongozi wa Serikali ya Rwanda una tuhuma za kujibu katika
Mahakama ya ICC, kuhusu mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Kongo.
Kauli hiyo ya Rapp inaunga mkono madai ya mara kwa mara
ya mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu ya
Human Right Watch, Save the Children, UNICEF na UNHCR, ambayo kwa nyakati
tofauti yamekuwa yakidai kuwa na ushahidi wa kutosha wa waasi wa M23 kusaidiwa
na Jeshi la Rwanda kufanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia katika miji
mbalimbali ya Mashariki mwa Kongo.
Inadaiwa pia kuwa upo ushahidi unaoonyesha jinsi ambavyo
waasi wa M23 wamekuwa wakiwatumia watoto wadogo katika vikosi vya majeshi na
ndio ambao wamekuwa wakitangulizwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano,
hususan katika matukio ya uhalifu wa kivita.
Tuhuma nyingine zinazoelekezewa Serikali ya Kigali ni
kufadhili kundi la waasi la CNDP, lililokuwa chini ya uongozi wa Jenerali Bosco
Ntaganda, ambaye amejisalimisha kwenye Mahakama ya ICC mapema mwaka huu.
Sehemu kubwa ya wapiganaji wa kundi la Ntaganda sasa
wameungana na waasi wa kundi la M23 na wamekuwa wakijiimarisha kiulinzi katika
maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini nchini Kongo.
0 comments:
Post a Comment