Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ameingilia kati ugomvi uliopo kati ya Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kaghasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba,
Dk. Anatoli Amani, kwa kuwataka wakae chini na kumaliza tofauti zao kwani
hakuna lisilokuwa na mwisho.
Rais aliyasema hayo katika uwanja wa Kaitaba alipokuwa
akihitimisha ziara yake mkoani Kagera aliyoanza Jumatano wiki iliyopita.
“Mbunge na Meya wakiendelea kutiliana shaka wanaoumizwa ni
wananchi, malizeni tofauti zenu kwa sababu hakuna lisilokuwa na mwisho,”
alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema masuala yaliyokuwa
yakiwagonganisha Meya na Balozi Kaghasheki ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini, ya
ujenzi wa soko pamoja na viwanja ni mambo ya maendeleo.
Katika ugomvi huo, Kaghasheki anapinga ujenzi wa soko jipya
mjini Bukoba kwa madai kwamba haukufuata maamuzi ya vikao vya Baraza la
Madiwani wakati Meya akisisitiza ujenzi huo kwa maelezo kwamba maamuzi ya
ujenzi yamepitishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani.
Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko ni suala la maendeleo lakini
akataka Manispaa iwatafutie eneo wajasiriamali wanaoendesha biashara zao kwenye
soko la sasa ambalo litavunjwa na kujengwa jipya.
Rais Kikwete aliagiza kuwa baada ya ujenzi, wananchi wanaondesha
biashara zao katika soko hilo wapewe kipaumbele.
“Ujenzi wa soko ni maendeleo na karne hii ni ya teknolojia, ni
uamuzi mwema; mkitaka mambo ya zamani basi na nyinyi mtakuwa ni watu wa
kizamani,” alisema.
“Katika mradi huu mpya wa viwanja 5,000 kwanza wapeni hao 800 wa
zamani maana walikwishalipia hilo ni deni la manispaa wala haliwezi kukwepeka
hata kama viongozi wa sasa hawakuwapo wakati huo,” alisema Rais Kikwete.
Balozi Kagasheki pamoja na mambo mengine alizungumzia kero ya
soko kuwa imeleta malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na kutofuatwa kwa
baadhi ya taratibu ikiwamo waliomo kutojua watahamishiwa wapi wakati soko hilo
likijengwa na muafaka wao baada ya ujenzi.
Kuhusu ardhi, alisema viwanja 5,000 vilivyopimwa havifahamiki na
kwamba baadhi ya wananchi hawakupewa fidia na wengine walilipwa kidogo na
kwamba wanaodai viwanja ni 800 na walikwishalipa tangu mwaka 2003.
Alisema Manispaa inawataka wananchi hao kuongeza fedha ndipo
wapewe viwanja vilivyopimwa katika mradi wa sasa.
Mgogoro kati ya viongozi hao ulianza baada ya uongozi wa Manispaa
kutangaza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa soko jipya na
la kisasa na upimaji wa viwanja 5,000.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rwekiza,
alisema bei ya kahawa inayotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo
(KNCU), haikidhi mahitaji ya wakulima.
Kadhalika, alizungumzia utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na
aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein ya ujenzi wa barabara ya Bukoba
–Bugabo Rubafu yenye urefu wa kilometa 42 lakini bado haijajengwa.
Kero nyingine alitaja kuwa ni mradi wa umeme vijijini akieleza
kuwa baadhi ya vijiji havikuingizwa kwenye mpango wa Wakala wa Umeme Vijijini
(REA), Kivuko cha Kyanyabasa, pamoja na mradi wa maji vijijini kwamba kati ya
vijiji 10 ni kimoja tu kilichotengewa fedha.
Akijibu hoja ya barabara na kivuko, Waziri wa Ujenzi, Dk. John
Magufuli, alisema itatengewa fedha pindi zitakapopatikana na kwamba kuhusu
kivuko, serikali inaangalia utaratibu wa kujenga daraja.
Kuhusu kero ya maji, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe,
alisema vijiji tisa vilivyotajwa na mbunge viko kwenye bajeti na kuzitaka
halmashauri kutekeleza miradi ya vijiji vyote na kwamba wananchi watachangia
baadaye.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, alisema ni dhamira ya serikali kuviunganisha vijiji vyote kwa umeme
ifikapo mwaka 2015.
Rais ameziagiza halmashauri zote nchini kutatua kero ndogondogo
za wananchi kama ushuru wa mazao kwa kuwa ziko ndani ya uwezo wao badala ya
kumsubiri yeye.
Aliwaonya maofisa wa serikali kuanzia ngazi ya vijiji, vitongoji
na kata kuacha biashara ya kutoa vibali kwa wahamiaji haramu.
Rais Kikwete amemaliza ziara yake mkoani Kagera aliyoianza
Jumatano iliyopita na anatarajiwa kuondoka leo kurejea Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment