Image
Image

BALOZI IDDI AZUNGUMZA NA WAWEKEZAJI KUTOKA JIMBO LA XIAMEN



 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Wawekezaji  10 kutoka Jimbo la Xiamen Nchini  Jamuhuri ya Watu wa China ofisini wake Vuga Mjini Zanzibar.


Zanzibar tayari imeshajitayarisha na kujiimarisha vyema kimiundo mbinu kwenye sekta tofauti katika azma yake ya kutoa fursa kwa wawekezaji na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi kuwekeza ndani ya Visiwa vya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza  hayo wakati wa mazungumzo yake  na Ujumbe wa wawekezaji kumi kutoka Jimbo la Xiamen Nchini Jamuhuri ya Watu wa China aliokutanao nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa wawekezaji  10 wa vitega uchumi kutoka Jimbo la Xiamen Nchini china mbele ya jengo la Ofisi yake vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif aliueleza ujumbe huo wa Manispaa ya Xiamen  ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Manispaa hiyo  Bwana Li Xiaoping kwamba Zanzibar imejipanga kujiimarisha kiuchumi kwa kutumia rasilmali ilizonazo ili kunyanyua mapato ya Taifa sambamba na ustawi wa jamii yake.

Alisema yapo maeneo kadhaa ya kilimo, uvuvi, utalii na hata viwanda vya uzalishaji  wa samaki na matunda ambayo yanaweza kutumiwa na wawekezaji hao ili kusaidia harakati za Maendeleo.

“ Tumeshuhudia jinsi Jamuhuri ya Watu wa China ilivyopiga hatua za haraka za maendeleo ya kiuchumi katika kipindi kifupi. Zanzibar imelenga kuiga mfano huo wa ndugu zetu wa china hata kama kwa kuanzia hatua za awali zilizofikiwa na Taifa hilo kubwa Barani Asia “. Alifafanua Balozi Seif.

Aliuhakikishia ujumbe huo wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada kwa wawekezaji wa Nchi hiyo watakaokuwa tayari kutaka kuwekeza vitenga Uchumi vyao hapa Zanzibar.
Alieleza kwamba Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar zina historia ya muda mrefu katika ushirikiano wa masuala ya kiuchumi, kibiashara pamoja na utamaduni.

Balozi Seif alitoa mfano wa  ushirikiano wa pande hizo mbili mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kuwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Sukari Mahonda, Viatu Mtoni, na Sigireti Maruhubi uliofanywa kwa msaada wa Serikali ya China ambao ulikuwa chachu ya kutoa ajira kwa kiwango kikubwa Nchini.

Balozi Seif alisema Zanzibar inajivunia harakati zake za kiuchumi inazopiga kutoka na kuungwa mkono na  china hasa  katika masuala ya ujenzi wa majengo tofauti na bara bara chini ya wahandisi kutoka Makampuni tofauti za Kimataifa za ujenzi za China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wahandisi wa Makampuni hayo kwa umahiri wao wanaochukuwa ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukibadilisha haiba ya Visiwa vya Zanzibar zaidi katika maeneo ya Miji yanayoonekana kujengwa majengo ya Ofisi za Serikali na Biashara.

Balozi Seif alifahamisha kwamba kufanikiwa kwa maendeleo makubwa ya Jamuhuri ya Watu wa China kunatokana na nguvu kazi inayochukuliwa na kila mwananchi wa Taifa hilo.

Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa wawekezaji kumi kutoka Jimbo la Xiamen Nchini China Mkurugenzi Mkuu wa Manispaa hiyo Bwana Li Xiaoping alisema ujumbe wake umeridhika na kufarajika na maeneo waliyopata nafasi ya kuyatembelea.

Bwana  Xiaoping alisema hatua hiyo itawapa fursa ya kuchambua na hatimae kuamua maeneo watakayoweza kuja kuwekeza hapa Zanzibar ikiwemo sekta ya Kilimo, Viwanda, Uvuvi, umeme pamoja na utalii.

Ujumbe huo umekuja Nchini kwa agizo la Rais wa China Bwana Xi Jinping kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliyoifanya Nchini China hivi karibuni na kufanya mazungumzo na wawekezaji mbali mbali wa Taifa hilo.

Mbali na ziara ya maeneo mbali mbali ya uwekezaji vitega uchumi hapa Zanzibar  lakini pia ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana kwa mazungumzo na kubadilishana mawazo na wafanyabiashara wa hapa Zanzibar.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment