Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi
mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qi Man, nyumbani kwake Mbweni. Balozi Chen
alikutana na Maalim Seif kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa
utumishi nchini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
amesema anasikitishwa na matukio ya hujuma yaliyojitokeza Zanzibar, ikiwemo
watu kumwagiwa tindikali, na kutaka uchungunguzi wa kina ufanywe kuwabaini
wahusika, na baadaye ripoti ya uchunguzi huo iwekwe wazi kwa wananchi.
Amesema hatua ya kuwekwa bayana ripoti za uchunguzi wa matukio
hayo ya hujuma, ni jambo muafaka katika kufuta dhana zinazojengeka miongoni mwa
wananchi na jamii ya kimataifa kuhusiana na watu wanaohusika kufanya hujuma
hizo.
Maalim Seif ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya
maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake mwaka
1964.
Amesema ili amani na mshikamano wa wazanzibari udumu, matukio
kama hayo ya hujuma ambayo yamekuwa yakiwalenga zaidi baadhi ya viongozi wa
dini na hata wageni, hayanabudi kuangaliwa kwa upana wake, na kuwataka wananchi
wajiepushe na kufikia maamuzi ya haraka kuwahusisha wengine bila ya uchunguzi
wa kina kufanywa.
Alisema wananchi walipata matumaini ya kukomeshwa kwa vitendo
hivyo mara baada ya hujuma zilizofanywa dhidi ya viongozi wa dini pamoja na
mripuko uliotokea katika kanisa la Arusha ambapo walihidiwa uchunguzi wa kina
utafanyika na kuhusisha wapelelezi wa kimataifa, lakini hadi sasa hakuna ripoti
yoyote iliyowekwa bayana.
Maalim Seif ameeleza kwamba badala yake matukio ya hujuma
yameendelea na wananchi kuendelea kujenga dhana ya kuwahusisha watu au makundi
maalum bila ya kuwa na uthibisho, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na utulivu
wa nchi.
“Ingekuwa wakati ule tungesema ni siasa, lakini sasa tuna
serikali ya pamoja Zanzibar, kwa nini mambo haya yanatokea sasa, huu ni mtihani
mkubwa kwetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF,
amesema pia amekuwa mgumu kuamini kuwa dini inahusika katika matukio ya hujuma
yaliyotokea Zanzibar.
Amesema Zanzibar ina historia ya kipekee ya uvumilivu wa kidini
duniani, kutokana na wananchi wa visiwa hivi kuishi pamoja kwa miaka mingi bila
ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
“Sisi Zanzibar kiwango chetu cha uvumilivu ni kikubwa na nambari
moja duniani, hata ukiangalia Ukristo Afrika Mashariki mlango wake ni
Zanzibar”, alifafanua Maalim Seif.
Akitoa mfano wa uvumilivu huo, Maalim Seif amesema hata unafika
mwezi wa Ramadhan huwezi kumuona mtu wa imani yoyote akila hadharani wakati wa
mchana, na kwamba wananchi wote wanashirikiana katika shughuli za kijamii bila
ya kujali imani zao.
Ameeleza kuwa baada ya matukio ya kujeruhiwa Padri Ambrose
Mkenda, kuuawa kwa Padri Evarist Mushina mripuko wa bomu katika kanisa mjini
Arusha, Serikali iliahidi kuleta makachero wa F.B.I, na hata baada ya wasichana
wa Kiingereza kumwagiwa tindikali inaelezwa wachunguzi kutoka Scktland Yard
wapo, lakini hakuna taarifa hadi sasa iliyotolewa kuhusiana na uchunguzi huo.
“Tusiajiegemeze kwenye dhana, uchunguzi ndio kitu muhimu. Hawa
wanaoathirika na hujuma mbali ya kuwa viongozi wa dini nao ni binadamu,
tujiulize jee hawakujenga uhasama au kutokufahamiana na wengine huko katika
jamii”, alihoji Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa ni makosa kuendesha mambo kwa dhana, kwa vile
matokeo yake ni kuwaadhibu watu kwa kuwaweka ndani bila ya kuwa na hatia.
Amewataka wananchi kuwa makini na waendelee kuwa wamoja, ili
amani, mashirikiano na umoja uliodumu uendelee wakati huu ambapo Zanzibar
inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
Wakati huo huo
Maalim Seif amekutana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar
Chen QiMan na kuelezea umakini na uadilifu wa makampuni ya Kichina katika kutekeleza
majukumu yao.
Amesema mara nyingi kazi za kiufundi wanazopewa wataalamu wa
Kichina zimekuwa zikitekelezwa kwa umakini na kwa wakati uliopangwa, hali
inayotoa matumaini ya kuendelea kutoa tenda kwa makampuni hayo.
Aidha amesifu ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na
Zanzibar ambao umekua ukichangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa
jamii.
Amemtaka balozi huyo kuwa kiungo katika kuwashajiisha watalii na
wawekezaji wa China kuja Zanzibar, ili kuendelea kuunga mkono juhudi za
serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema China ni mshirika wa kweli wa maendeleo ambayo imekuwa
ikishirikiana na Zanzibar katika kutatua kero zinazoikabili ikiwa ni pamoja na
kusaidia wataalamu hasa katika sekta ya afya.
Naye balozi QiMan amesema katika kipindi chake cha utumishi hapa
nchini, ameshuhudia mafanikio makubwa yakipatikana yakiwemo kuimarika kwa
majengo, huduma za elimu pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma
Abdulhabib Ferej akipokea zawadi kutoka kwa Balozi mdogo wa China aliyepo
Zanzibar Chen Qi Man, wakati wakiaagana kufuatia balozi huyo kumaliza muda wake
wa utumishi nchini.
Ameahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Zanzibar na
kutoa michango zaidi katika kusaidia uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Balozi
Chen QiMan amemaliza muda wa utumishi hapa nchini, baada ya kuitumikia nafasi
hiyo ya ubalozi mdogo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.




0 comments:
Post a Comment