MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba
(CCM), amechafua hali ya hewa bungeni kwa kuitaka Serikali kuwachukuliwa hatua
viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mbunge
huyo alisema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu
wake, Dk. Wilbroad Slaa, wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa madai ya kusababisha
mauaji ya raia.
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Bara, alisema katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi
ilipotoka kwenye uchag
uzi, viongozi hao wamekuwa wakihamasisha maandamano na
kusababisha umwagaji wa damu za Watanzania.
“Mheshimiwa Naibu Spika, katika
kipindi cha miaka miwili tangu nchi yetu ilipomaliza Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakitoa kauli za wazi na hata kusababisha
mauaji ya watu bila hatia.
“Kutokana na hali hii, sijui Serikali inafanya nini
katika kuwachukulia hatua, kwani viongozi hawa wamekuwa wakitafuta umaarufu wa
kisiasa kwa kuchochea chuki na mauaji dhidi ya raia.
“Kwa hali hiyo, tangu
kipindi hicho hadi leo hii wanasubiri nini badala ya kwenda kuwaweka jela,
kwani huko ndiko wanatakiwa kuwa,” alisema.
Mwigulu, alisema kukosekana kwa
maadili kwa baadhi ya viongozi wa siasa, ambao wamekuwa wakitumia majukwaa na
kuhubiri umwagaji damu ni hatari kwa taifa.
Alisema viongozi hao wamekuwa
wakitumia majukwaa hayo na kusababisha vifo vya wananchi, huku akitaja vurugu
zilizotokea katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na Singida.
Akijibu swali
hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alisema
Serikali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kukusanya
ushahidi na kwamba mahakama ndicho chombo chenye uamuzi wa mwisho dhidi ya
adhabu kwa raia au kiongozi yeyote wa kisiasa.
Kauli hiyo ya Mwigulu
ilionekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Bunge, ambapo Mbunge wa Nyamagana,
Ezekiel Wenje (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akimtaka
Mwigulu kuthibitisha kauli yake, vinginevyo aombe radhi.
Wenje alisema hoja ya
Mwigulu imekosa mashiko na ina lengo la kuwadhalilisha viongozi wa Chadema,
huku akisahau kuwa baada ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki, aliyekuwa Mwenyetiki
wa Chadema tawi la Usa River, Omari Mbwambo, aliuawa na watu anaodaiwa kuwa ni
wafuasi wa CCM.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne
Kilango (CCM), alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa wanasiasa
wanaokiuka maadili na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Wanataaluma kama vile
madaktari, wahandisi, wahasibu na hata wakandarasi pindi wanapokiuka maadili ya
kazi zao huchukuliwa hatua kwa kufutiwa leseni zao.
“Vile vile viongozi wa
kisiasa wanayo maadili yanayowaongoza, kwanini pale wanapokiuka maadili ya kazi
zao hawachukuliwi hatua kama ilivyo katika makundi hayo? (taaluma),” alisema
Kilango.
CHANZO MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment