Mlinzi aliyeuawa alisahahu kufunga lango
la chumba cha Simba huyo.
Mfanyakazi mmoja wa hifadhi ya wanyama amefariki baada
ya kushambuliwa na Simba katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, baada ya
kusahau kufunga lango la chumba cha mnyama huyo.
Simba huyo anayeitwa Kenenisa, ambalo ni jina la
mwanariadha mashuhuri Kenenisa Bekele, alimuuma Abera Silsay, 51, shingoni,
wakuu wa hifadhi hiyo wanasema.
Shambulio hilo linasemekana kudumu kati ya dakika
15-20
Hifadhi hiyo ilifunguliwa mwaka wa 1948 kuwalinda
Simba waliokuwa wamefugwa na kiongozi wa zamani wa Ethiopia, Haile Selassie.
Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza akiwa mjini Addis,
anasema alipozuru hifadhi hiyo saa kadhaa baada ya tukio hilo la Jumatatu
asubuhi, kiatu cha mwanaume huyo aliyeuwawa kilikuwa bado kwenye sakafu, kando
ya Simba huyo mwenye umri wa miaka saba.
Hifadhi hiyo ilifungwa siku nzima kwa umma. Maafisa
wanasema takriban watu 2000 hutembea hapo kila siku.
Walinzi walijaribu kumshutua Simba huyo kwa kufyatua
risasi hewani lakini juhudi zao ziliambulia patupu, mwandishi wetu anasema.
Bwana Abera alishambuliwa alipokuwa akisafisha chumba
cha simba huyo
Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Dkt Musie Kiflom
anasema mfanyikazi huyo alikuwa amedumu kwa mwaka mmoja tuu katika kazi hiyo na
hakuwa na uzoefu mkubwa ikilinganishwa na wafanyakazi wenzake.
"Aliingia chumba nambari 10 ambapo Kenenisa
hulala na alisahau kufunga lango la chumba anakolala simba huyo” Musie Kiflom
aliliambia shirika la habari la AFP.
"hatimaye, simba huyo alikuja na kumvamia,"
alisema.
Bwana Musie aliwaambia wanahabari kuwa polisi waliitwa
kujaribu kusaidia, lakini ilikuwa “ vigumu sana kumsaidia mwenzetu”.
Bwana Abera alifariki papo hapo, aliongezea.
Hifadhi hiyo ni makao ya simba 15 wa Uhabeshi, ambao
wamo hatarini
Simba hao huwekwa katika nyumba zilizofungwa lakini
wakuu wanasema mipango inaendelea kuwahamisha hadi nyingine ambayo ni kubwa
zaidi katika miezi 13 ijayo.
Hii ni mara ya pili kwa mfanyakazi wa kutunza simba
katika kituo hicho katika kipindi cha miaka 17, kwa mujibu wa shirika la habari
la AFP.
Hifadhi hiyo sasa itaimarisha mafunzo kwa wafanyikazi
wote baada ya tukio hilo.
BBC
0 comments:
Post a Comment