WATANZANIA wametakiwa kumuenzi
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu JK. Nyerere kwa kuchukia vitendo vya uhalifu na
wahalifu vinavyotokea katika jamii ili kuhakikisha taifa la
Tanzania linaendelea kuwa la amani, Usalama na utulivu kuanzia
ngazi ya familia hadi Taifa.
Hayo yalibainishwa na Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso wakati akijibu
swali lililomtaka yeye kama mwanausalama anataka watanzania wamuenzi
namna gani muasisi wa taifa la Tanzania kwani yeye alikuwa ni
kiongozi wa amani kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Akimzungumzia Baba wa Taifa, Senso
alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye msimamo imara, alikuwa
anachukia vitendo vya vyote vya ubadhilifu, unyanyasaji, uchochezi wa kidini,
kisiasa ikiwa ni pamoja na vitendo vya uhalifu, vitu ambavyo ni hatari
kwa taifa linalohitaji ushirikiano wa pamoja baina ya Serikali na wananchi wake
ili liweze kujikwamua kimaendeleo hususani kiuchumi, kisisasa yakiwemo
maendeleo ya kiulinzi na usalama.
Alibainisha kuwa, miongoni mwa
mbinu za kupata maendeleo ya kiusalama ni ushirikiano wa jamii katika kubaini
na kufichua uhalifu na wahalifu katika makazi yao kwa kutoa taarifa kwa Jeshi
la Polisi au kushirikiana na askari tarafa waliokwisha sambazwa katika tarafa
kote nchini ili kushirikiana na familia katika kutatua kero za kiusalama
zinazowakabili.
“familia zikiwa salama, tutakuwa
na mtaa salama, Mitaa ikiwa salama, tutakuwa na kata salama, Kata zikiwa salama
tutakuwa na tarafa salama, Tarafa zikiwa salama tutakuwa na Wilaya salama,
Wilaya zikiwa salama, tutakuwa na Mikoa salama, Mikoa ikiwa salama, Tutakuwa na
Taifa salama” alisema Senso.
Pia alitoa wito kwa wananchi
kutowaonea haya wahalifu badala yake waendelee kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu kwa kuwa kosa la jinai huwa halifutiki, taarifa hizo ni muhimu kwani
zitasaidia kukamatwa kwa wahalifu waliotenda uhalifu katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Aliongeza kuwa mhalifu ni
adui namba moja wa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla kwani unyang’anya
au kuiba mali za mtu au umma ambazo zimepatikana kwa taabu, jambo
ambalo hata baba wa taifa alikuwa akilikemea kwani linarudisha nyuma maendeleo.
Na. Tamimu Adam, Jeshi la Polisi.


0 comments:
Post a Comment