:TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na mwaka mpya, wananchi wenye imani ya
Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na
muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe ambapo uzoefu
unaonyesha baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya
uhalifu hasa wa kujipatia vipato na mali.
Kufuatia hali
hiyo, Jeshi la Polisi nchini, katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna
vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kipindi hiki cha sikukuu na pale
ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo
yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote
ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Hata hivyo, watu wote watakaoenda
maeneo ya beach wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kuzama kwenye maji.
Aidha,
tunawakumbusha wananchi kuwa makini
katika suala zima la usalama wa maisha na mali zao, hususani kuchukua hatua
stahiki na za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya
uhalifu katika maeneo yao na sehemu mbalimbali za biashara, na watokapo kwenye
makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na pale inapobidi watoe taarifa
kwa majirani zao. Wazazi wanakumbushwa kuwa makini na watoto kwa kutokuwaacha
watembee peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha
madhara juu yao ikiwemo kupotea. Aidha, wazazi waepuke kuwapeleka watoto kwenye
kumbi za disko toto ambazo siyo salama.
Vilevile,
wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie usalama katika kumbi zao, hawarusiwi
kujaza watu kupita kiasi kwenye kumbi hizo, hususani kumbi za disko toto.
Aidha, wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa
ya watu wanakumbushwa kufunga vifaa maalum vya kufuatilia mienendo ya watu
wanoingia na kutoka katika maeneo hayo (CCTV kamera).
Pia, Jeshi la
Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa
makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa
magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.
Mwisho, tunawaomba
wananchi waendelee kutoa taarifa za mipango yoyote ya uhalifu watakayoiona
ikiendelea mahali popote kwa kuwafichua wahalifu hao ili hatua za kuzuia
uhalifu huo ziweze kuchukuliwa mapema. Taarifa zinaweza kutolewa kupitia namba
ya simu 0754 78 55 57 au Simu za
Makamanda wa Polisi wa mikoa au katika kituo chochote cha Polisi.
0 comments:
Post a Comment