Na.Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah
Jasmine Kairuki na Mke wa aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Graca Machel
wametoa wito kwa wadau kutoka taasisi za umma na binafsi kuunganisha nguvu ili
kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu na kuondokana na ndoa za utotoni.
Bi. Machel, kupitia asasi yake inayojulikana na
Mfuko wa Graca Machel (Graca Machel Trust), yupo nchini Tanzania kwa ziara
rasmi ya kikazi kuunga mkono jitihada za serikali na taasisi mbalimbali
zilizopo nchini kupiga vita ukeketaji na ndoa za utotoni.
Tangu mwezi Agosti 2014, Mfuko wa Graca Machel
kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali ya ‘Children’s Dignity Forum
(CDF)’ na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Idadi ya Watu
Duniani (UNFPA), wamekuwa wakianzisha na kuendesha miradi mbalimbali inayolenga
kumaliza ndoa za utotoni katika mkoa wa Mara ambao matukio ya ndoa za utotoni
yanaelekwa kuwa mengi.
Miradi hiyo ni pamoja na mafunzo kuhusu athari
za ndoa za utotoni na ukeketaji kwa maofisa wa Mahakama, Polisi, viongozi wa
kidini na kimila pamoja na walimu na wanafunzi.
Akiongea jijini Dar es Salaam jana (Jumatano,
Januari 21, 2015), Bi. Machel amesema ingawa serikali na wadau wengine
wamefanya jitihada kubwa ili kumaliza ukeketaji na ndoa za utotoni, lakini
vitendo hivyo bado vinaendelea na hivyo kuhitajika mkakati unaojumuisha wadau
wote ili kuondokana na matatizo hayo yanayotokana na tamaduni potofu.
“Baadhi ya tamaduni zinaweza kubadilishwa,
hususan pale zinapodhuru watu, jamii na taifa,” alisema Bi. Machel na kuongeza
kuwa nguvu za pamoja zinahitajika kutoka ngazi za chini kabisa.
“Hebu tujaribu kuunda umoja wenye nguvu ili
kumaliza ndoa za utotoni. Umoja ambao unajumuisha wadau wa sekta ya umma na
binafsi, viongozi wa kimila na kidini, shirikisho la walimu na asasi za
kiraia…hili jambo lisiwe la mtu mmoja, liwe letu sote!’ alisema Bi. Machel
anayetambulika kama mwanaharakaiti wa kimataifa wa haki za watoto.
Bi.Machel, ambaye taasisi yake inajihusisha na
haki za wanawake; haki za watoto; na demokrasia na utawala bora, alisisitiza
kuwa umoja huo unapaswa kuwa na mipango mathubuti inayotekelezeka wakati wote
hata pale kunapokuwa na mabadiliko ya uongozi wa katika wilaya au vijiji.
Akiongea katika mkutano huo, Naibu Waziri
Kairuki alimshukuru Bi. Machel kwa jitihada zake na kumhakikishia kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha
kuwa watoto wote, hususan wa kike wanapata elimu na ndoa za utotoni na vitendo
vya ukeketaji vinamalizika mkoani Mara na nchini kote.
Naibu Waziri alimweleza Bi. Machel, ambaye
aliambatana na Mwakilishi wa UNFPA hapa nchini Dkt. Natalia Kanem na Mkurugenzi
Mtendaji waCDF Bw. Koshuma Mtengeti kuwa haki za watoto zimejumuishwa katika
Katiba Inayopendekezwa. Aidha, Naibu Waziri Kairuki aliongeza kuwa serikali
imeongeza jitihada za kutoa elimu kwa watoto wa kike na jamii kwa ujumla
kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na vitendo vya ukeketaji.
Kairuki pia alimweleza Bi. Machel namna katiba
mpya inatakavyoisadia serikali katika kusimamia sekta muhimu kama elimu ili
kuwawezesha watoto wote, wakiwemo wa kike, kupata haki zao ikiwemo haki ya
kupata elimu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, ili
mafanikio makubwa yapatikane, ni muhimu kuwa na mikakati inayojumuisha watunga
sera, viongozi wa kidini na jamii zinazojihusisha na vitendo vya ukeketaji na
ndoa za utotoni.
Bi. Machel alitarajiwa kuondoka leo (Alhamisi,
Januari 22, 2015) kwenda mkoani Mara kukagua utekelezaji wa miradi ambayo
inatekelezwa kwa pamoja kati ya serikali, CDF na UNFPA.
0 comments:
Post a Comment