TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JK:
Asilimia 90 ya watoto wote wanapata chanjo
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa
asilimia 90 ya watoto wote wa Tanzania sasa wanapata chanjo kutokana na kazi
inayofanywa na taasisi ya kusambaza chanjo duniani ya Global Alliance for Vaccines and Immunisazation (GAVI).
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa bila kazi hiyo ya GAVI ni dhahiri kuwa baadhi ya nchi
duniani hasa zile zinazoendelea zingekuwa zinapoteza watoto wengi mno duniani
kutokana na magonjwa ambayo yanazuilika kabisa kwa njia ya chanjo.
Rais Kikwete
ameyasema hayo, Jumanne, Januari 27, 2015, wakati alipohutubia mkutano mkubwa
unaojadili chanjo na jinsi ya kuchangia fedha zaidi za kuboresha mpango huo wa
chanjo kwa watoto unaofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Berlin
Congress Centre katika mji mkuu wa Ujerumani wa Berlin. Rais Kikwete ni miongoni
mwa viongozi wawili wanaoliwakilisha Bara la Afrika katika mkutano huo.
Kiongozi mwingine ni Rais Babacar Keita
wa Mali.
Akihutubia
mkutano huo asubuhi ya leo, Rais Kikwete ameorodhesha mafanikio makubwa ambayo
Tanzania imeyapata katika kuokoa watoto wake kwa sababu ya matumizi makubwa ya
chanjo zinazotolewa chini ya mpango na
kazi ya GAVI.
Rais Kikwete
amefafanua: “Uzoefu wetu katika Tanzania ni kuwa kazi ya GAVI ina manufaa makubwa.
Katika Tanzania pekee yake, GAVI inasambaza aina 11 za chanjo ambazo
zimepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Tanzania ni moja ya nchi
zinazofanya vizuri zaidi katika chanjo katika eneo la Kusini mwa Sahara ambako
asilimia 90 ya watoto wanapata chanjo.”
Ameongeza: “Mwaka
2013 pekee yake, asilimia 104 ya watoto walipata chanjo ya ugonjwa wa TB, asilimia
80 walipata chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu, asilimia 91 walichanjwa kwa
ugonjwa wa polio, asilimia 99 kwa ugonjwa wa tetekuwanga.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Kwa msaada wa GAVI, mpaka Oktoba
mwaka jana, watoto 20,529,629 kati ya umri wa miaka tisa na 14 walikuwa wamepata
chanjo na walitakiwa kupata chanjo ya ugonjwa huo.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Watoto 9,291,119 sawa na asilimia 100 walipatiwa vitamin A na watoto
asilimia 76 walipewa dawa za kukabiliana na minyoo na hivyo kuongeza ubora wa
maisha ya watoto wetu.”
Baadaye, Rais
Kikwete ameshriki katika mkutano na waandishi wa habari ambako amejiunga na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya GAVI Dagfin Hoybraten, Mtendaji Mkuu wa
GAVI Dkt. Seth Berkley, Mwenyekiti mwenza wa Mfuko wa Bill and Melinda
Foundation Bwana Bill Gates, Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa
Ujerumani Dkt. Gerd Muller na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Save the Children
International Bi. Jasmine Whitbread.
Rais Kikwete
alitarajiwa kuondoka Berlin, Ujerumani kwenda Paris, Ufaransa baada ya ziara ya
siku mbili katika mji mkuu huo wa Ujerumani.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
29 Januari, 2015
0 comments:
Post a Comment