Sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti
ya Tegeta Escrow linaweza kuwa limefanya jina la Profesa Sospeter Muhongo
kuzungumzwa sana na kuonekana amekuwa kwenye wakati mgumu tangu lilipoibuka,
lakini ukweli ni kwamba lilikuwa hitimisho tu la matukio mengi tangu msomi huyo
aanze kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
Muhongo, ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya
Kikwete kuwa mbunge Mei 3, 2012 kabla ya kufanya mabadiliko kwenye Baraza la
Mawaziri, amekuwa kwenye kiti moto wakati wote tangu ashike uwaziri kutokana na
kashfa ambazo hazikomi kwenye sekta ya madini na nishati, na tabia yake ya
kushambulia wanaotoa hoja kwa maneno ya dhihaka na kujisifu, ambayo mara nyingi
yalikera watoa hoja.
Mikataba 26
Waziri Muhongo alianza kazi kwa kuliagiza
Shirika la Mafuta (TPDC) kupitia upya mikataba 26 ya utafutaji gesi, hatua
ambayo iliungwa mkono na wengi huku wakitaka ripoti ya kazi hiyo iwe bayana ili
Watanzania wajue uozo uliopo, hata hivyo, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi
huo, Profesa Muhongo hakuweka bayana matokeo ya ripoti hiyo, badala yake
akasema ripoti hiyo itatumika wakati wa kuingia mikataba mipya tofauti na
alivyoeleza mwanzo kuwa angefuta mikataba mibovu.
Akajikuta anaingia kwenye mzozo na wadau,
hasa wabunge, na miaka miwili baadaye, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
ikaiagiza menejimenti ya TPDC kupeleka mikataba hiyo kwenye kamati, lakini
menejimenti ikagoma, kitendo kilichosababisha viongozi wa shirika hilo
wakamatwe.
Kampuni ya Puma Energy
Hatua iliyozua tafrani zaidi ni ile ya wizara
yake kuipa kampuni ya Puma Energy zabuni ya ugavi wa mafuta mazito kwa kampuni
ya kufua umeme ya IPTL. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa, hasa bungeni ambako
watunga sheria walidai kuwa zabuni hiyo ilitolewa bila ya kufuata Sheria ya
Manunuzi. Wabunge walidai kuwa Puma Energy haikuwemo kati ya kampuni
zilizoomba, na kutuhumu kuwa kulikuwa na rushwa.
Wabunge walitaka Profesa Muhongo na katibu
wake, Eliackim Maswi wawajibishwe, hoja iliyosababisha mgawanyiko mkubwa
bungeni kiasi cha CCM kuitisha kikao cha wabunge wake kupanga mikakati ya
kumuokoa waziri huyo.
Katika sakata hilo, Profesa Muhongo aliingia
kwenye mgogoro na mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye
alichangia hoja. Katika majibu yake, Profesa Muhongo alisema kuwa alikuwa
akidhani mbunge huyo kuwa ni msomi, na akalazimika kufuatilia elimu yake.
Alipotaka kueleza matokeo ya kidato cha nne ya Ole Sendeka, Spika Anne Makinda
alimzuia na kumtaka aendelee na hoja iliyokuwa mbele yake.
Wafanyabiashara wazawa
Tabia ya Profesa Muhongo kujibu hoja kwa kushambulia
walioitoa iliamsha mjadala mkubwa baada ya wafanyabiashara wakubwa kulalamika
kuwa wizara hiyo haitoi kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa leseni za
utafutaji gesi na mafuta. Katika kujibu hoja hiyo, mtaalamu huyo wa jiolojia,
aliwaita wafanyabiashara hao kuwa ni madalali na hawana uwezo wa kufanya kazi
hiyo.
Alieleza kuwa kazi hiyo inahitaji mtaji
mkubwa. Alisema maombi tu ya kazi hiyo yanagharimu Dola 700,000, wakati takwimu
za kazi hiyo zinagharimu Dola 3 milioni, utafutaji Dola 15,000 hadi 20,000 kwa
mita moja ya mraba, kuchoronga kwenye kina kirefu kuna gharimu Dola 1 milioni
kwa siku, wakati kumaliza tundu moja ni Dola 1 na yanahitajika matundu 12.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment