Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama
Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutokubali kuuza maeneo ya ufukwe
wa Bahari ya Hindi kwa kiasi kidogo cha fedha kwani thamani ya
maeneo hayo ni kubwa.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea kwa nyakati
tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama
hicho katika matawi ya Raha leo na Ufukoni yaliyopo katika kata ya
Rahaleo wilayani
humo.
Alisema hivi sasa kuna wageni
wengi ambao wanaenda kwa wananchi na kununua maeneo ya ufukweni kwa bei ya
chini lakini kama wamiliki wa maeneo hayo watakuwa na subira
watayauza kwa bei kubwa kwa kipindi cha miaka
michache ijayo.
“Baada ya miaka michache ijayo mkoa wetu utakuwa
tofauti kimaendeleo, Serikali inampango wa kujenga mji wa kisasa
katika eneo la Mitwero.
“Nawasihi hata kama mtu
anashida kiasi gani atafute njia nyingine ya kupata fedha lakini siyo kuuza eneo la ufukweni kwa
bei ndogo, kama kuna aliyebakiza eneo lake asiuze kwani
kimfaacho mtu ni chake”, alisisitiza Mama Kikwete .
Kuhusu elimu MNEC huyo aliwasihi viongozi hao kusimamia
elimu ya watoto wao na kuwahimiza waende shule kwani wakiwa na elimu
wataweza kufanya kazi za kitaalamu katika sekta mbalimbali ikiwemo ya gesi
inayopatikana mkoani humo.
Kwa upande wa wanawake
aliwahimiza kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika
uchaguzi mkuu ujao na hivyo kufika katika ngazi ya
maamuzi pia kwa kufanya hivyo hawatapoteza haki yao ya msingi ya
kuchaguliwa.
Akiwasalimia viongozi hao Mkuu wa wilaya ya Lindi Dkt.
Nassoro Hamidi alisema shule za Sekondari zimefunguliwa lakini wanafunzi
walioripoti shuleni ni wachache na kuwaomba kupita nyumba hadi
nyumba kuwahamasisha wazazi wawapeleke watoto wao shule kwani bila ya elimu
hakuna maendeleo.
“Serikali ilitoa
agizo kama watoto hawana ada au nguo za shule waende hivyo hivyo kuanza masomo
mambo mengine yatafuata baadaye lakini hadi sasa bado idadi ya wanafunzi
walioripoti shuleni ni ndogo”, alisema Dkt. Hamidi.
Kuhusu wananchi kujitolea
katika ujenzi wa maabara aliwasihi viongozi kuwahimiza kushiriki katika
ujenzi na maabara hizo ziweze kukamilika kwa wakati ili watoto
wajifunze masomo ya sayansi kwa vitendo.
Mama Kikwete yupo wilayani
humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya
vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 . Hadi
sasa ameshatembelea matawi 64 kati ya 82 yaliyopo wilayani humo.
0 comments:
Post a Comment