Image
Image

Rais Kikwete – Uongozi siyo kujisifu


                            TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa uongozi siyo kujisifu na kujisifia tu bali ni kutenda vitendo na kufanya maamuzi yanayothibitisha na yanayolingana na sifa hizo.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Februari 10, 2015, wakati alipofungua jengo la kisasa kabisa la kitega uchumi lenye thamani ya sh. bilioni 64 kwenye Manispaa ya Moshi katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku mbili ya kikazi Mkoani Kilimanjaro.

Jengo hilo linalojulikana kama Kilimanjaro Commercial Complex na lililoko katikati ya Manispaa ya Moshi limejengwa kwa ubia wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii la NSSF, taasisi ya Girls Guide Tanzania,  taasisi ya Red Cross na Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) na ndilo jengo kubwa kuliko yote katika manispaa hiyo.

Amelisifia uongozi na visheni ya maamuzi ya NSSF akisisitiza kuwa shirika hilo limethibitisha kwa vitendo sifa ambazo shirika hilo linazo na zimethibishwa. “Uongozi siyo kujisifia na kujisifu tu bali ni kutenda vitendo na kufanya maamuzi yanayothibisha na kulingana na sifa hizo na katika hilo NSSF imeonyesha njia.”

Jengo hilo ambalo ujenzi wake ulianza Desemba 2011 na kuchukua miaka mitatu limejengwa kwa pamoja na Kampuni ya Group Six International ya China na Advent Construction ya hapa nchini na litakuwa na maduka makubwa na madogo, maofisi, mabenki na kumbi za mikutano.

Akizungumza katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi na viongozi wa taasisi zilizoko katika ubia wa ujenzi wa Jengo hilo, Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudencia Kabaka amesema kuwa ni muhimu kwa NSSF kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati na inayolipa, badala ya fedha hizo kubakia kwenye mabenki tu ambako zinaweza kukumbwa na athari za mfumuko wa bei.

Mapema, Rais Kikwete katika shughuli yake ya kwanza baada ya kuwasili Mkoani Kilimanjaro, alifungua wodi ya upasuaji na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la wodi ya akinamama na mtoto katika Hospitali ya Mkoa ya Mawezi katikati ya Manispaa ya Moshi. Mawenzi ni moja ya hospitali kongwe zaidi nchini ikiwa imeanzishwa mwaka 1920

Akizungumza kabla ya kufanya shughuli hizo mbili kubwa, Rais Kikwete ameelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Sera ya Afrika ya mwaka 2007 iliyochukua nafasi ya sera ya mwaka 1997, ikiwa ni pamoja na kujenga maabara za kisasa katika kila hospitali ya Mkoa nchini na kuzifanya hospitali hizo kuwa za rufani ndani ya mikoa.

Rais Kikwete pia ameelezea jitihada za Serikali kupambana na magonjwa mbali mbali ikiwemo malaria na ukimwi na juhudi za kupunguza vifo vya watoto na akinamama kwa sababu ambazo zinazuilika.

Aidha, Rais amefafanua hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya ambazo ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya kufundishia madaktari katika hospitali mbili kubwa na mpya za Mlongazila na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na upanuzi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhas cha Dar es Salaam.

Rais Kikwete pia amezungumzia matatizo ya kudumaa kwa watoto wadogo nchini akisema kuwa matunzo na lishe ya watoto wadogo katika siku 1,000 za kwanza za maisha yake ni muhimu sana katika maisha ya baadaye ya watoto.

Amesema kuwa kwa watoto wadogo lishe duni inasababisha kudumaa kwa watoto, watoto kuwa na kimo kidogo kuliko umri wao, watoto kuwa na uzito mdogo kulinganisha na umri wao, watoto kuwa na upungufu wa madini joto na upungufu wa vitamin A.

Rais Kikwete ataondoka kesho kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara hiyo.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

10 Februari, 2015




Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment