OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip
Saliboko, anayetuhumiwa kupata mgawo wa Sh milioni 40 za Akaunti ya
Tegeta Escrow, ametumia mbinu zilizotumiwa na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM), kukwepa kuhojiwa na Baraza la Maadili ya
Viongozi wa Umma.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Chenge kukataa kuhojiwa na
Baraza hilo Februari 25, mwaka huu, akisema kuna zuio la Mahakama Kuu
linalokataza suala hilo kujadiliwa na chombo chochote.
Baada ya pingamizi hilo, Februari 26, mwaka huu, Baraza hilo lilitoa
hukumu ndogo juu ya pingamizi hilo na kusema zuio la Mahakama Kuu
halilizuii kujadili suala hilo.
Sababu ya pili ya Baraza kutupilia mbali pingamizi hilo, ni kutokana na
kile lilichosema zuio la Mahakama Kuu kuzuia mjadala huo ambao matokeo
yake yatafanya jambo hilo lijadiliwe kwenye Bunge la Jamhuri ya
Muungano, jambo ambalo halitatokea kwa baraza hilo kumhoji mtuhumiwa.
Hata baada ya maelezo na msimamo huo wa Baraza, Chenge alikataa kuhojiwa
na kutaka kwenda Mahakama Kuu kutafuta tafsiri ya zuio hilo.
Njia hiyo ya Chenge kukwepa mkono wa Baraza hilo, ndiyo iliyotumiwa na
Saliboko jana ambaye baada ya kusomewa mashtaka yake aliyakana.
Baada ya kuyakana, wakili wake, Jamhuri Johnson, aliomba kutojadiliwa na
Baraza hilo kwa madai kuna zuio la Mahakama Kuu linalokataza shauri
linalohusu Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL) na miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow kujadiliwa.
“Pamoja na kuwa kwenye shauri la Chenge, Baraza hili lilisema lina uwezo
wa kusikiliza shauri hili na kwamba lenyewe siyo sehemu ya zuio lililo
Mahakama Kuu, tunasema kwamba zuio lililo Mahakama Kuu linahusu vyombo
vya umma, na hili Baraza ni chombo cha umma.
“Kwahiyo tukatafsiri kwamba, ‘by necessary implication’, kama vyombo
vingine vya umma vimezuiwa kujadili hili suala, basi na hili Baraza
limezuiwa kwa sababu ni chombo cha umma,” alisema.
Baada ya kusema hayo, wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, Hassan Mayunga, alipinga pingamizi hilo kwa madai kuwa Baraza hilo
lilishatolea ufafanuzi suala hilo.
Alisema Baraza hilo ni chombo kinachojitegemea na kwamba hakiwezi kuzuiwa kulijadili suala hilo.
“Amri hiyo si zuio la dunia nzima na wala halizuii watu wengine, bali
mwanasheria anatengeneza kichaka kukwepa majukumu yake ya kisheria,”
alisema Mayunga.
Baada ya mabishano ya mawakili hao, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji
mstaafu Hamis Msumi, aliitupilia mbali hoja ya wakili wa Saliboko.
Katika kuitupa hoja hiyo, Jaji Msumi alisoma tena hukumu ndogo aliyoitoa alipokuwa akiamua pingamizi la Chenge.
Jaji Msumi alisema zuio la Mahakama Kuu, mkazo uliwekwa katika kulijadili suala hilo na kusababisha liwasilishwe bungeni.
Alisema kutokana na hali hiyo, pingamizi hilo halina msingi, kwani pia
Baraza hilo linajitegemea na huru na siyo kati ya vyombo vilivyozuiwa na
mahakama hiyo kujadili suala hilo.
MASHTAKA YA SALIBOKO
Akisoma mashtaka yanayomkabili Sariboko, Wakili wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Mayunga, alisema mlalamikiwa amekiuka
maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa fungu la 12 (1) e, 12 (2) na
fungu la 6 (f) ya sheria ya maadili ya mwaka 1995.
“Mlalamikiwa aliomba fadhila za kiuchumi kutoka kwa James Rugamalira
kinyume cha fungu la (6) (f) ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya
mwaka 1995, ambalo linamzuia kiongozi wa umma kuomba au kupokea fadhila
za kiuchumi,” alisema.
Alisema mlalamikiwa alipokea Sh 40,429,000 kutoka Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited.
“Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya mlalamikiwa iliyoko Benki ya
Mkombozi, tawi la St. Joseph, Dar es Salaam, akaunti namba
00420102645501, Februari 5 mwaka 2014,” alisema.
Alisema mlalamikiwa kwa wadhifa wake wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Ufilisi (Rita), aliteuliwa na Mahakama Kuu kuwa mfilisi wa muda wa mali
za IPTL, kampuni ambayo VIP Engineering and Marketing Limited ilikuwa
inamiliki hisa asilimia 30.
“Kitendo cha mlalamikiwa kupokea Sh 40,429,000 kutoka kwa Kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited, iliyokuwa na hisa kwenye Kampuni ya
IPTL, wakati mlalamikiwa akiwa mfilisi wa mali za IPTL, ni ukiukwaji wa
fungu la 6 (e) la sheria ya maadili ya viongozi wa umma, ambalo
linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgogoro wa masilahi,”
alisema.
Alisema mlalamikiwa kwa kutumia wadhifa wake, alijipatia manufaa ya
kifedha kinyume na fungu la 12 (1) (e) la sheria ya maadili ya viongozi
wa umma.
“Mlalamikiwa hakutamka jumla ya Sh 40,429,000 alizopokea kutoka kwa
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kinyume na matakwa ya
fungu la 6 (e) na fungu la 12 (2) la sheria ya maadili ya viongozi wa
umma,” alisema wakili Mayunga.
MUJUNANGOMA KUSUBIRI KESI YA KISUTU
Katika hatua nyingine, Baraza hilo limekubali pingamizi la kutosikiliza
kesi ya Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rogonzibwa Mujunangoma, hadi pale kesi ya jinaidi
kuhusu uchotwaji wa fedha hizo iliyo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
itakapokwisha.
Mujunangoma alifikishwa mbele ya Baraza hilo akidaiwa kujipatia manufaa
ya kifedha kiasi cha Sh 423,400,000 kwa ushauri anaoutoa katika Kampuni
ya VIP na Mabibo Beer Wines and Sprit kinyume cha sheria ya maadili ya
viongozi wa umma.
Pingamizi lake la kutojadiliwa na Baraza hilo kutokana na kuwa na kesi
inayohusu suala hilo mahakamani, lilikubaliwa jana baada ya Jaji Msumi
kusema hoja zilizotolewa na mlalamikiwa ni za msingi.
Jaji Msumi alisema hoja ambayo imeonekana kuwa na msingi wa kisheria
iliyochangia kulishawishi Baraza kukubali pingamizi hilo, ni ukweli
kwamba mashtaka yaliyoko Kisutu ndiyo yale waliyomfungulia katika Baraza
la Maadili.
“Sheria inakataa mshtakiwa kuwa na kesi katika sehemu mbili kwa wakati
mmoja yenye malengo yaleyale kwenye vyombo tofauti, inamkosesha nafasi
ya kujitetea,” alisema.
MASHTAKA
Kabla ya pingamizi lake kukubaliwa, Mujunangoma alikuwa akikabiliwa na
mashtaka ya kutoa ushauri wa kisheria katika Kampuni ya VIP na Mabibo
Beer Wines and Sprit kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma
na kujipatia manufaa ya kifedha kiasi cha Sh 423,400,000.
Pia kuingiziwa fedha katika akaunti yake yenye namba 00120102602001
iliyopo kwenye Benki ya Mkombozi, Tawi la St. Joseph, Dar es Salaam.
Kwa kitendo cha mlalamikiwa kuwa mshauri wa Kampuni ya VIP Engineering
and Marketing Limited ambayo ilikuwa na hisa za asilimia 30 katika
Kampuni ya IPTL ni kujiingiza katika migongano ya kimaslahi.
Kosa jingine ni mshtakiwa kutotamka masilahi aliyokuwa nayo katika
mkataba wa Tanesco na IPTL kupitia Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited kinyume cha matakwa ya kifungu cha 14 cha sheria ya
maadili.
Mlalamikiwa kutotamka madeni yake aliyokuwa anaidai Kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited na Mabibo Beer Wines and Sprit kwa
kamishna wa maadili kwa kipindi cha mwaka 2013 kinyume na matakwa ya
kifungu cha 9(6)(b) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Sorce:Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment