Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza kuwa mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa waliyonayo wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza, akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.” Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
Alisema mtandao huo utamuunga mkono mwanamke yeyote atakayeonyesha nia ya kugombea bila kuangalia itikadi ya chama anachotoka, huku ukiamini kuwa wanawake wanaweza kufanya vizuri zaidi wanapopata nafasi.
“Japokuwa historia inaonyesha wanafanya vizuri, tunahitaji kuwaunga mkono kwa nia thabiti ili wakalete mabadiliko ya kweli, ” alisema Liundi.
0 comments:
Post a Comment