Walimu 18,000 kupigwamsasa Mtaala mpya wa Elimu ili kuwajengea uwezo wa kufundisha Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi Darasa la kwanza na pili .
JUMLA ya walimu 18,000 wa shule za msingi kutoka mikoa 14 nchini wanatarajiwa kupatiwa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuweza kufundisha Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi Darasa la kwanza na pili .
Mafunzo hayo yatatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Jumanne Sagini, alisema mitaala ya mafunzo hayo imeandaliwa na TET kutokana na malengo ya Serikali ya kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
“Mafunzo haya yatatolewa kwa Walimu ambao watawezesha ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa watoto walio katika vituo vya Elimu nje ya Mfumo Rasmi.
“Walimu 4,430 kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Rukwa, Ruvuma, Morogoro na Pwani watashiriki mafunzo katika awamu ya kwanza,”alisema Sagini
Alisema walimu 4,492 watashiriki mafunzo katika awamu ya pili kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Katavi, Geita, na Mwanza.
Aidha, alisema walimu 9,078 watashiriki katika awamu ya tatu na ya nne ya mafunzo hayo.
” Walimu hao wanashiriki mafunzo chini ya mpango wa Serikali unaofadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu, (Global Partnership for Education-GPE).
“Mafunzo hayo yamepangwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma na awamu ya kwanza itaanza Aprili 13 hadi 21,awamu ya pili tarehe Aprili 27 hadi Mei 6 na awamu ya tatu Mei 11 hadi Mei 20 2015 na awamu ya nne itaanza Mei 25 Mei hadi Juni 3 mwaka huu,”alisema Sagini.
Alisema pia walimu kutoka mikoa 11 watapatiwa mafunzo chini ya mipango ya wahisani tofauti.
“Walimu wa mkoa wa Mtwara walishapatiwa mafunzo hayo chini ya Shirika la Maendeleo la Marekani –USAID; Mikoa ya Kigoma, Tabora, Lindi, Simiyu, Mara, Shinyanga na Dodoma wanaendelea kupatiwa mafunzo chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uingereza- DfID na mikoa ya Mbeya, Njombe, na Iringa watapata mafunzo chini ya ufadhili wa Shirika Watoto la Umoja wa Mataifa-UNICEF,”alisema.
0 comments:
Post a Comment