Na Modewji
blog team
SERIKALI na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jana wametiliana saini mkataba utakaowezesha
kutekelezwa kwa mradi wa kuwezesha walimu wa Tehama vyuoni nchini.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome
alisema mradi huo ni mkombozi mkubwa katika maandalizi ya kufundisha kwa
kutumia Tehama nchini.
Alisema mpango huo wenye kuwezesha walimu kujifunza
Tehama unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambao ndio
wamepitisha fedha zao UNESCO.
Katika utiaji saini huo ambapo Balozi wa China
nchini Dk. Lu Youqing alikuwepo, katika jumla ya uhai wa mradi ambao ni miaka
miwili , miundombinu ya ufundishaji masomo ya sayansi na hesabu katika vyuo vya
walimu vya Monduli na Tabora itaboreshwa.
Katika mradi huo walimu watafundishwa elimu ya
Tehama, namna ya kufundisha na kujifunza.
Katibu mkuu Mchome alisema kwamba vyuo hivyo viwili
vitawezeshwa kuwa na mtandao ambao utaunganishwa na vyuo vingine vinane vya
masomo ya sayansi na hesabu kwa ajili ya kubadilishana taaluma.
Pia vyuo hivyo vitawezeshwa kuandaa programu zenye
kuelezea mfumo wa utoaji huduma za Tehama kwa ajili ya walimu wa masomo ya
sayansi na hesabu.
Profesa Mchome alisema ili taifa liweze kusonga
mbele katika mpango wake wa kufundisha kwa kutumia Tehama ni vyema kuandaa
walimu na fedha za China kupitia Unesco zitasaidia maandalizi hayo.
“Tunaamini tukiwekeza katika vifaa vya kupromoti
Tehama, walimu wakifundishwa na kuandaliwa vyema, wataenda kusaidia kufundisha
na kuwezesha matumizi ya Tehama katika shule zao.” Alisema Profesa Mchome.
Alisema japo zipo program ndogo nyingine , program
waliyotia saini jana ilikuwa kubwa na yenye tija itakayoimarisha ubora wa elimu
kwa kuwapa wanafunzi elimu ya kujitegemea, elimu yenye kuwakwamua kiujuzi na
kuutumia ujuzi huo kwa maendeleo yao na taifa.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa barani Afrika
ambayo mapema wametambua thamani ya kufundisha kwa njia ya Tehama ili kuboresha
elimu na mfumo wa elimu.
Taasisi zitakazohusika na mradi huo ni pamoja na
Chuo Kikuu Huria (OUT) na Taasisi ya Elimu nchini(TIE) kwa kuratibiwa na Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
0 comments:
Post a Comment