Shughuli za kuadhimisha siku ya
mazingira Duniani zimeanza rasmi leo hii na mwaka huu kauli mbiu ni 'Ndoto
bilioni saba. Sayari Moja. Tumia kwa kujali.'
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki-Moon, lengo kwa mwaka huu ni kukuza suala la maendeleo endelevu,
ili kuboresha hali ya maisha kwa wote duniani bila ya kuchochoe uharibifu wa
mazingira, na bila ya kuhatarisha raslimali zinazohitajika kwa vizazi vijavyo.
" Kuanzia mwaka huu tujitahidi tuwe
waangalizi bora wa dunia yetu," amesema Ban.
Ban aliongeza katika mwaka huu wa
mabadiliko, kuna mategemeo ya kusonga mbele katika masuala ya maendeleo
endelevu na mabadiliko ya tabia nchi. Amesisitiza siku ya leo iadhimishwe kwa
kuwa waangalifu zaidi, juu ya athari zetu kama binaadamu juu ya viumbe na
mazingira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa mpango wa
mazingira wa Umoja wa Mataifa, Achim Steiner, amesema katika maisha ya dunia
hii ya utandawazi yenye watu bilioni 7, ni rahisi sana kupuuza athari za
binaadamu juu ya mazingira.
Aliendelea kwa kusema kuwa maadhimisho
haya ya kila mwaka, yanawakumbusha watu dunia nzima kuwa ni uwamuzi wetu sisi
binadamu ambao unaijenga dunia.
"Maamuzi yetu na matumizi yetu ya kila
siku ya mabilioni ya watu yana athari kwa mazingira. Baadhi ya matumizi ya kila
siku yanachangia katika kupungua kwa maliasili, lakini baadhi pia ya vitendo
vya binaadamu vinasaidia kuhifadhi mazingira. Sasa uwamuzi ni wetu sisi,"
amesema Steiner.
Jukumu la kila mmoja ya watu bilioni saba
Steiner amesema matumizi mabaya
yasiyokuwa endelevu pamoja na uzalishaji wa viwanda, ni miongoni mwa sababu
kubwa za uharibifu wa mazingira.
Hakuna shaka kuwa katika miaka 50
iliyopita tumeona mabadiliko makubwa ya mahusiano baina ya wanaadamu na
mazingira yaliyomzunguka, hususan katika ongezeko la matumizi yasiyo endelevu
ya maliasili, ambalo limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Steiner amesema angependa kila mmoja
kufikiria dunia itakuwa wap,i ikiwa kila mmoja kati ya watu bilioni 7
atachangia katika kuleta mabadiliko ya matumizi bora ya raslimali yenye busara.
Wito wake ni kwa kila mmoja kujitahidi kutekeleza hilo, hata kama ni kwa
kukataa kutumia mifuko ya plastiki ama kupanda baiskeli badala ya gari ama basi
kwenda kazini.
0 comments:
Post a Comment