MMOJA wa makada 39 wa CCM waliojitosa kuwania kuteuliwa na chama
hicho kuwania urais wa Tanzania baadaye mwaka huu, Boniface Ndembo jana
alirudisha fomu huku akilalamikia hali ya rushwa, akisema ni mbaya na
kwamba kuna baadhi ya maeneo watu walitishia kumkataa kumdhamini kama
asingetoa fedha.
Ndembo ambaye ni mmoja wa wagombea waliorejesha fomu jana, alisema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari. Mwingine aliyerudisha
fomu ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe.
Chikawe alirejesha fomu kimya kimya. Aidha, Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani naye alirejesha fomu . Ndembo alisema
ni lazima ifike mahali suala la rushwa likome.
“Changamoto kubwa niliyoikuta mahali ambapo nimepita kama mgombea ni
kuona jinsi ambavyo rushwa ilikuwa imetawala inatia hofu juu ya taifa
inapokwenda,” alisema.
Alisema katika mchakato wake wa kuzunguka mikoani ameshuhudia na
kuona watanzania na wananchi wa kawaida ni sehemu ya zao la rushwa.
“Kuna mahali unafika watu wanakataa kukudhamini kwa vile huna fedha
za kuwapa wanakuambia waziwazi mbona fulani alitupa fedha na wewe lazima
utoe…
“Sijajua kwa nini baadhi ya wagombea wanaandikwa sana kwenye magazeti
wakati wa kutafuta wadhamini na wengine hawaandikwi, kuna wakati
nimekumbana na hilo na nikapata changamoto,” alisema.
Alisema ifike mahali Watanzania wakaachana na rushwa hasa katika
mambo yanayoligusa taifa kama kutafuta kiongozi wa nchi ili apatikane
kiongozi asiyehusishwa na rushwa.
Alisema rushwa imekuwa adui mkubwa na nchi itaweza kupata kiongozi anayetokana na rushwa jambo ambalo ni hatari kubwa.
“Mahali pengine unaambiwa mbona fulani katoa kiasi fulani hiyo ni
changamoto kubwa ya kupata viongozi wanaotokana na rushwa, waandishi wa
habari wakiwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa jambo
hilo litafanikiwa,” alisema.
Alisema waasisi wa taifa hili waliweka misingi mizuri na hakukuwa na
matabaka ya mwenye nacho na asiye nacho, lakini misingi hiyo itaondolewa
na watu wanaotafuta uongozi wa nchi kwa kutumia rushwa.
Alisema CCM ni chama chenye mfumo wa demokrasia bila kujali nyadhifa
ma nafasi zao katika jamii. Alisema ameweza kuzunguka mikoa 15 ikiwemo
12 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya Zanzibar.
Alisema amefanikiwa kupata wadhamini 602. Naye Dk Kamani ambaye
amekuwa Mwanachama wa nane kurudisha fomu ya kuomba kuchaguliwa na chama
hicho akizungumza na waandishi wa habari mara alisema amezunguka jumla
ya mikoa 17 huku 14 ikiwa ni ya Tanzania Bara na 3 ikiwa ni ya Tanzania
Visiwani.
Alisema aliamua kutafuta wadhamini katika maeneo ya vijijini ili
aweze kujua matatizo yanawakabili ili aweze kuyatatua pindi atakapopewa
ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kama atapewa nafasi ya kuwa Rais atahakikisha anajikita
katika kilimo kwani anaamni ndio kutapunguza pengo la mtu aliyenacho na
yule ambaye hana.
‘’Sina cha kuficha mimi ni mtu safi na ninajiamini ndio maana hata
kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Simiyu,nawaomba mniombee
ili niwe Rais wenu nitatue matatizo ya Watanzania pamoja na suala la
rushwa ambalo kwetu limekuwa janga kubwa’’alisema Dk Kamani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment