Wadau hao walisema kwa hali ilivyo sasa,na kwa kuzingatia unyeti
wa miswada yenyewe,hawaoni sababu ya kuwa na haraka ya kupitisha
miswada hiyo katika Bunge la 10, mkutano wa 20 unaoendelea mjini Dodoma.
Hoja yao kuu ni kutaka miswada hiyo isubiri serikali ijayo ili ipate
nafasi ya kuchambuliwa kwa kina na kufanyiwa marekebisho kwa umakini ili
mwishowe iwe na maslahi mapana kwa taifa.
Wadau hao wa mafuta na gesi walitoa msimamo huo mjini Dodoma juzi
katika mkutano uliohusisha pia Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini,
Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Bajeti.
Wakati wakichangia, baadhi ya wadau akiwamo Mbunge wa Igunga na
aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini nchini, Dalali Kafumu, alisema kuna
kasoro kadhaa katika miswada hiyo na hivyo haipaswi kupelekwa haraka.
Alitaja baadhi ya kasoro hizo kuwa ni muswada huo kunakili karibu kila
kitu kutoka katika muswada kama huo nchini Uganda ikiwamo tafsiri ya
baadhi ya maneno isiyoeleweka vyema.
Siyo nia yetu kutaka kujadili yaliyomo ndani ya miswada hiyo. Hata
hivyo, sisi tunaona kwamba ni kweli, kuna kila sababu ya kuruhusu
mijadala ya kina miongoni mwa wadau kabla ya kufikia hatua ya kuifikisha
bungeni.
Tunashauri jambo hili huku tukijua kwamba sheria zinazotumika sasa
ni za miaka ya 1980 na 2008, ambazo kwakweli bado zina maeneo kadhaa
yasiyotoa suluhu ya moja kwa moja kwa changamoto mbalimbali zitokanazo
na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia na pia mifumo ya kiuchumi
duniani kote.
Hata hivyo, pamoja na yote hayo, sisi tunadhani kwamba ni vizuri
dhamira yoyote nzuri kuhusiana na namna bora ya kusimamia rasilimali za
mafuta na gesi isiruhusu kuwapo kwa maamuzi ya pupa.
Ikumbukwe kuwa tunakoelekea, taifa letu litakuwa likitegemea uchumi
wake kukua kwa kasi kubwa zaidi kupitia sekta ya gesi na mafuta. Tafiti
katika maeneo mbalimbali nchini zimethibitisha kuwa hadi kufikia sasa,
taifa lina rasilimali ya gesi asilia ya futi za ujazo zaidi ya trilioni
50.
Zipo pia tafiti nyingine nyingi zinazotoa matumaini ya kupatikana
kwa kiwango kingine kikubwa zaidi cha rasilimali ya gesi na mafuta. Kwa
sababu hiyo, sekta hii inatarajiwa kuwa mhimili mkuu wa kiuchumi.
Itaingiza mapato ya moja kwa moja kupitia kodi, mauzo ya gesi na mafuta
ughaibuni, kutoa ajira, kuwezesha ustawi wa viwanda nchini na pia
kufanikisha uzalishaji wa mbolea utakaoongeza uzalishaji wa chakula.
Hakika, zipo faida nyingi zitokanazo na gesi na mafuta na hivyo, hakuna
ubishi kuwa hii ni sekta muhimu na nyeti kwa maslahi ya taifa ambalo
kufikia mwaka 2025 linatarajiwa kuwa la uchumi wa kati.
Kwa kuzingatia yote hayo, sisi tunaona kwamba ni kweli, kuna kila
sababu ya kujipa muda wa kutosha katika kujadili masuala ya gesi na
mafuta.
Aidha, kuna ukweli kuwa wabunge wengi hivi sasa hawana utulivu wa
kutosha kiasi cha kuweza kujadili kwa kina miswada hii. Na hili liko
wazi. Kwamba huu ni mkutano wa mwisho kwao na hivyo kifikra, wengi wao
hawako bungeni hata kama wanaonekana kimwili. Wengi wanawazia hatma yao
katika uchaguzi. Na wengi wao hawaonekani bungeni Dodoma kwa sababu
wangali wakiweka mambo yao sawa kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika
Oktoba. Ushahidi ni kuwapo kwa mahudhurio ya chini mno katika baadhi ya
vikao, kimojawapo kikiwa ni kile kilichokuwa na wabunge 68 tu kupitisha
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha
2015/2016, badala ya zaidi ya 300.
Katika mazingira kama hayo, hatuoni uwezekano wowote wa kuwa na
wabunge wenye kujadili mambo kwa kina kama tuliowazoea. Ni kwa sababu
hawana utulivu.
Ni katika mazingira kama haya, ndipo nasi tunapoona kuwa miswada
hii inayohusu gesi na petroli haipaswi kupelekwa bungeni wakati huu.
Tuzingatie.
0 comments:
Post a Comment