Image
Image

SPIKA MAKINDA:Mkionyesha njaa mtajishushia heshima.

Wakati Muswaada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2015 ukipitishwa jana bungeni, Spika, Anne Makinda ameitaka Serikali na wabunge kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma, kwani itawajengea heshima.
Akihitimisha mjadala huo uliopitishwa kwa kifungu kwa kifungu, Makinda alisema: “Mkiwa na nidhamu ya matumizi ya fedha mtaheshimika na mkionyesha njaa, mtajishushia heshima.”

Hata hivyo, Makinda aliipongeza Kamati ya Bajeti kwa kazi waliyoifanya, huku akisisitizia kuwa Spika ajaye atakuta tayari kuna sheria ya fedha ambayo inasisitizia nidhamu ya matumizi yake.

Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha Muswada huo ili Bunge liliruhusu matumizi ya fedha za bajeti zilizopitishwa hivi karibuni pamoja na tozo za kodi zilizopendekezwa.

Katika michango yao, wabunge wengi walionyesha hofu kuwa hata kama Serikali itajitahidi kukusanya fedha, bado matumizi yake hayaridhishi hali inayoifanya ionekane kama ‘inatwanga maji kwenye kinu’.

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCS Mageuzi), David Kafulila alisema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania ni Serikali kushindwa kudhibiti matumizi ya rasilimali zake.

Kafulila alilalamikia pia suala la matumizi ya bidhaa feki ambazo alidai zinaipunguzia hadhi Serikali, kwa madai kuwa haina ubavu wa kuwadhibiti watu wanaozingiza nchini.

“Pamoja na hayo, nimelalamikia na kuomba miongozo mara kadhaa hapa lakini sijapata majibu ya kutosha kuhusu kiasi cha Sh238 bilioni ambazo zinahusishwa na kuagizwa kwa mabehewa hewa na bando 1,000 za mabati bandia lakini hakua anayejali,” alilalamika Kafulila na kuongeza:

“Mimi naamini hakuna uthubutu ndani ya Serikali, mnaishia kuwaogopa watu na hasa kampuni kubwa mnaziogopa sana, igeni mfano wa Mkurugenzi wa Bahati Nasibu (Abbas Tarimba) ambaye akikamata mashine bandia, anazichomwa moto hadharani,” alisema Kafulila.

Kwa upande wake, Rajabu Mohamed Mbarouk (CUF), alisema kuna mianya mingi inayotumika katika ukwepaji wa kodi inayowapa nafuu wafanyabiashara wakubwa wakati wadogo wakiendelea kubanwa.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliiambia Serikali iache kigugumizi kwani wafanyabiashara wanaokwepa kodi inawajua na ndiyo maana imekuwa ikipiga kelele kuwa wako wakwepa kodi wakubwa.

Godbless Blandes (Karagwe - CCM), aliitaka Serikali kuondoa ushuru na kodi katika maji. Mbunge huyo alisema binadamu yeyote lazima anywe maji na hiyo siyo starehe, hivyo kuyawekea kodi ni sawa na kutaka kuwaumiza wananchi wake.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment