Awali, ilitarajiwa kwamba uandikishaji huo
ungekamilika kabla ya Aprili 30, siku iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya upigaji
wa Kura ya Maoni lakini mashine za uandikishaji za BVR zilichelewa na
kusababisha mchakato huo kusuasua.
Hivi sasa Tume iko katika maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu na tayari imeshasema utafanyika Oktoba 25. Kama ilivyo kwa Kura
ya Maoni, Uchaguzi Mkuu nao utategemea kukamilika kwa uandikishaji huo.
Makadirio yanasema kuwa wanaotarajiwa
kuandikishwa ni watu 24 milioni. Kwa siku 96 kuanzia Februari 24 hadi Mei 31,
wameandikishwa watu milioni sita tu na kwa mujibu wa ratiba ya Tume
uandikishaji unapaswa kukamilika Julai 18, hivyo ndiyo kusema kuwa zimesalia
siku 44 tu kuandikisha watu zaidi ya milioni 18.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu la Taifa
(NBS), inakadiriwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wapatao milioni
2.9. Hao wanatarajiwa kuandikishwa katika Daftari kwa siku 12 tu kuanzia Julai
4 hadi 16. Sababu inayotolewa na NEC ni kuwa eti mashine zote 8,000 za BVR kwa
wakati huo zitakuwa Dar es Salaam jambo ambalo halina uhalisia kwani wakati huo
ndipo mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga itakuwa inaendelea na uandikishaji.
Takwimu za NBS zinakadiria kuwa Morogoro ina
watu wanaostahili kupiga kura wapatao 1.28 milioni wakati Tanga ina wapigakura
wapatao 1.12 milioni. Hao wote kwa ujumla wao ni sawa na watu milioni 2.4 idadi
ambayo ni ndogo kuliko ya wapigakura wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini huko
wamepewa mwezi mzima wa uandikishaji.
Kwa mtiririko huo wa mambo, hatuoni jinsi
ambavyo NEC itakamilisha uandikishaji kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hofu hiyo wanayo
Watanzania wengi, lakini kama kawaida Tume imekuwa bingwa wa kuweka nta
masikioni.
Tunaitaka iongeze kasi ya uandikishaji ili
kuwapa matumaini Watanzania hasa kwa sababu uzoefu unatuonyesha kuwa katika
maeneo ambayo tayari uandikishaji umekamilika ilibidi ziongezwe siku kwa sababu
wapigakura waliojitokeza ni zaidi ya makadirio.
Hivyo, kwa makadirio yasiyo rasmi yawezekana
wapigakura wakawa zaidi ya milioni 27. Kama hivyo ndivyo, NEC inabidi ijipange
upya na iweke nguvu zaidi kukabiliana na changamoto hiyo, kinyume chake
kuandikisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku 44 zilizosalia ni ndoto. Hata
kama ikibadili ratiba na kusema itaandikisha mpaka Oktoba 24 bado siku hizo
hazitoshi kutokana na mwenendo wenyewe wa uandikishaji unavyoendelea.
Hadi sasa bado malalamiko ya misururu mirefu
katika vituo vya uandikishaji yanaendelea sambamba na waandikishaji kuchukua
zaidi ya nusu saa kuandikisha mtu mmoja, hali hiyo inadhihirisha kuwa tumefanya
makosa kufanya jambo kubwa kama hili la uandikishaji upya wapigakura mwaka wa
uchaguzi.
Mambo yamekuwa mengi, tumejizonga na
kuzongeka na sasa joto la wasiwasi linazidi kupanda. Ndiyo maana tunasema
tunapaswa kutafuta mpango B mapema kabla hatujaenda mrama.
0 comments:
Post a Comment