Taarifa iliyotolewa na EWURA jijini Dar es Salaam jana ilitaja bei
mpya elekezi ya rejareja itakayotumika kuanzia leo Julai 1, 2015 kuwa ni
petroli iliyoongezeka kwa Sh. 232 kwa lita sawa na asilimia 11.82,
dizeli imeongezeka kwa Sh. 261 kwa lita (asilimia 14.65) na mafuta ya
taa yameongezeka kwa Sh. 369 wka lita, sawa na asilimia 22.75.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, ilieleza kuwa miongoni mwa sababu
zilizoongeza bei ya mafuta ni kuendelea kudhoofu kwa thamani ya shilingi
dhidi ya dola ya Marekani na pia mabadiliko ya tozo za serikali katika
mafuta kuanzia Julai Mosi mwaka huu (leo).
Kadhalika, taarifa hiyo ya Ngamlagosi ilieleza kuwa bei za jumla
kwa mafuta hayo zimeongezeka pia, petroli ikipanda kwa Sh. 232.35 kwa
lita sawa na asilimia 12.49, dizeli Sh. 261.15 kwa lita sawa na asilimia
15.57 na mafuta ya taa Sh. 369.41 kwa lita, sawa na asilimia 24.32.
“Kulinganisha na thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani kwa
machapisho ya bei za mwezi Juni na Julai 2015, shilingi imepungua
thamani kwa shilingi 175.11 kwa dola ya Marekani sawa na asilimia
8.65,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Ngamlagosi.
BEI HALISI
Taarifa ya EWURA ilieleza kuwa kufuatia mabadiliko hayo, bei
elekezi ya rejareja ya petroli kwa mkoa wa Dar es Salaam ni Sh. 2,198,
dizeli Sh. 2,043 na mafuta ya taa Sh. 1,993.
Kadhalika, taarifa hiyo ilitaja bei elekezi katika kila mkoa,
ukiwamo wa Arusha ambao bei elekezi kwa lita moja ya petroli kuanzia leo
ni Sh. 2,282, dizeli Sh. 2,127 na mafuta ya taa Sh. 2,077, huku bei
elekezi ikionekana kuwa juu zaidi katika maeneo kama Bukoba ambako
petroli itauzwa Sh. 2,413, dizeli Sh. 2,258 na mafuta ya taa Sh. 2,208;
na Uvinza mkoani Kigoma bei ya petrol ni Sh. 2,441, dizeli Sh. 2,286 na
mafuta ya taa Sh, 2,236.
Taarifa hiyo ilibainisha vilevile kuwa vituo vyote vya mafuta
vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango
yanayoonekana wazi na kuonyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya
biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
SOKO LA DUNIA
Wakati bei ya petroli ikipanda nchini, hali iko tofauti katika soko
la dunia ambako bei ya mafuta ghafi imeendelea kushuka kila uchao.
Taarifa zinaonyesha kuwa Mei 1, 2015, bei ya pipa moja la mafuta
ghafi ya petroli lilikuwa likiuzwa kwa dola za Marekani 64.13. Hata
hivyo, bei hiyo imeendelea kuporomoka kila uchao na hadi kufikia Juni
22, pipa moja la mafuta ghafi ya petroli katikia soko la dunia lilikuwa
likiuzwa kwa dola za Marekani 60.54, sawa na punguzo la dola za Marekani
3.95, sawa na asilimia 5.93.
Kupungua huko kwa bei ya petroli katika soko la dunia hakuonyeshi
kuleta nafuu kubwa nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya
kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola. Takwimu za
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa kufikia Mei 29, 2015, dola
moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh. 2,007.08 huku wastani kwa
mwezi wote ikiwa ni dola moja ya Marekani kwa Sh. 1,955.72. Kufikia
jana (Juni 30, 2015), kwa wastani dola moja ya Marekani ilikuwa
ikibAdilishwa kwa Sh. 2,030.40, ikiwa ni kuporomoka kwa shilingi kwa
wastani wa asilimia 7.2 kulinganisha na Mei, 2015.
0 comments:
Post a Comment