Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli na Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan, jana walipata mapokezi makubwa jijini Dar es Salaam wakitokea mjini Dodoma.
Dk. Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho mjini
Dodoma Jumamosi iliyopita katika kinyang'anyiro cha urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba
25, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Dk. Magufuli alishinda kwa asilimia 87.1 dhidi
ya wagombea wenzake, Balozi Amina Salim (asilimia 10.5) na Dk.
Asha-Rose Migiro (asilimia 2.4).
KUWASILI DAR
Dk. Magufuli aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere saa 7:09 mchana na kupokelewa na Katibu wa Halmashauri
Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es
Salaam, Ramadhani Madabida, wabunge wa mkoa wa huo, Mkuu wa Mkoa, Said
Meck Sadik, Meya wa Jiji, Dk. Didas Masaburi, Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake Taifa (UWT), Sophia Simba, viongozi wa dini na makada wa ngazi
za juu wa CCM.
Baadhi ya wana-CCM waliomiminika kwenye Uwanja wa Ndege, walikuwa
wakiimba nyimbo za kumsifu na kumpongeza Dk. Magufuli na baadaye
alizungumza na makada wa CCM na wananchi waliojitokeza kumlaki.
Dk. Magufuli aliwashukuru wana-CCM waliojitokeza kumpokea na chama
hicho kwa kumteua kuwania nafasi hiyo huku akisisitiza kuwa
hatawaangusha.
Alisema mapokezi aliyoyapata katika Jiji la Dar es Salaam, ni
makubwa na hiyo ni dalili nzuri kuwa chama hicho kitaendelea kushika
dola kwa miaka mingi zaidi.
WAMUITA TINGATINGA
Wakati mgombea huyo wa urais akihutubia, baadhi ya wana-CCM waliojitokeza uwanjani hapo walisikika wakimuita `tingatinga.
Mara baada ya kupokewa, Dk. Magufuli alielekea katika ofisi za CCM
Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye kwenda viwanja vya Mbagala Zakhem
kulikokuwa kumeandaliwa kwa ajili ya mapokezi na kutambulishwa rasmi kwa
wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla.
MAMIA WATANDA BARABARANI
Akiwa njiani kuelekea ofisi za Chama Mkoa mtaa wa Lumumba, Polisi
wa Kikosi cha Usalama Barabarani walionekana wakiwa wametanda barabara
zote za makutano pamoja na makundi ya watu yakiwa yamesimama kando kando
ya barabara kutaka kumshuhudia.
Katika kituo cha daladala Mnazi Mmoja, hakukuwa na daladala na
abiria walijaa kituoni hapo wakiwa na shauku ya kumuona Dk. Magufuli.
OFISI ZA CCM MKOA
Mara baada ya kuwasili ofisi za CCM Mkoa , Dk. Magufuli alipokelewa
na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na kundi kubwa la wana-CCM na
wananchi wengine.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dar es Salaam,
Dk. Magufuli aliwaeleza kuwa wagombea wa CCM walikuwa 42 na jumla ya
makundi yalikuwa 42.
"Ni utaratibu wa kawaida kwenye chama kilichokomaa demokrasia
kupitia ngazi hiyo, lakini makundi hayo yamemalizika na sasa wamekuwa
kundi moja kwa ajili ya kuitangaza Ilani ya Uchaguzi ya CCM," alisema
Dk. Magufuli.
Aliongeza: “Nawashukuru wana-CCM kwa heshima waliyonipa kwa
kuniteua kupeperusha bendera ya chama changu, naamini mapokezi makubwa
niliyoyapata hapa yanadhihirisha ushindi mkubwa wa chama changu,
ninaahidi sitawaangusha na nitafanya kazi kwa nguvu zote na maarifa
yangu na yale mtakayonipa,” alisema Dk. Magufuli.
MGOMBEA MWENZA
Kwa upande wake, Mgombea mweza, Samia Suluhu Hassan, aliishukuru
serikali na chama hicho kwa niaba ya wanawake wote Tanzania, kwa
kuwateua wanawake kuanzia nafasi mbalimbali za chini hadi sasa nafasi ya
juu.
Jumamosi ya wiki iliyopita Dk. Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa
mkutano mkuu wa CCM, kuwania nafasi ya urais kupitia chama chake kwa
ushindi wa
ATANGAZA KIAMA KWA WASIOWAJIBIKA
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alisema kuwa ukali wake
utaonekana zaidi kwa watendaji wa serikali ambao kwa makusudi
wameshindwa kutimiza wajibu wao na hivyo kuongeza kero kwa wananchi na
kuahidi kwenda nao sambamba bila kuogopa wala kuonea mtu.
Akizungumza katika mkutano wa utambulisho wake na Mgombea Mwenza
Samia Suluhu Hassan, jana mchana katika viwanja vya Zakhiem, Mbagala,
Dar es Salaam, Dk. Magufuli alisema yeye siyo mkali, lakini kipimo cha
ukali wake kitaonekana kwa watendaji wa serikali ambao ni wazembe.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, alisema wakati anaomba
ridhaa ya chama chake, alipokutana na waandishi wa habari alipenda
kuwaambia:"Nawaomba Watanzania waniombee na hata siku ya kurudisha fomu
nilisema hivyo...Sala zimefika kwa Mungu na nimekuwa mteule."
“Sitawaangusha, nitafanyakazi kweli kweli, sitamuogopa mtu,
sitapenda mtu wa chini aonewe, machinga anasumbuliwa, bodaboda
anasumbuliwa...nitaisimamia vizuri serikali, kero ndogo zifutike kabisa,
leo najitambulisha ila nina mengi ya kuongea wakati wake ukifika
nitafanya hivyo,” alisisitiza.
Dk. Magufuli alisema Ilani ya CCM imezungumzia mambo mengi kama
kilimo, biashara na kuahidi kuwalinda wafanyabiashara wakubwa na wadogo
ili Watanzania wajiajiri.
Alisema maendeleo hayana chama na maendeleo ya kweli yatatokana na
viongozi wa CCM, kwa kuwa Mtanzania mwenye itikadi ya chama na asiye na
chama anachotaka ni maendeleo ya kweli.
AAHIDI KUSIMAMIA HAKI
Alisema kuwa atahakikisha anasimamia haki, umoja, maendeleo, viwanda, afya, barabara, reli, maji na kero nyingine zote.
“Nazungumza muda huu jua linawaka, Haki ya Mungu kweli tutafanya
kazi, tutafanya kazi, nawaomba wana-Dar es Salaam tukiamini Chama Cha
Mapinduzi, tupeni madiwani na wabunge wa CCM ili mafiga matatu yatimie,
ukiwa na tochi lazima iwe na betri tatu ukiweka gunzi katikati haiwezi
kuwaka,” alibainisha.
Alisema sura yake ni mbaya, lakini ni nzuri usiku na ya mgombea
mwenza ni nzuri, lakini kikubwa kinachoangaliwa na Watanzania ni kazi
ambayo anaahidi kuitekeleza ili kuondoa kero mbalimbali.
“Watanzania watarajie nchi huru na maendeleo bila kujali itikadi zao,” alisema.
Dk. Magufuli alisema ataendelea kulinda misingi ya Watanzania
iliyowekwa na waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume na
kuimarishwa na viongozi waliofuatia kwa pande zote za Muungano katika
kudumisha umoja na amani.
“Umoja ni ushindi ndiyo maneno yetu kwa sasa, tupo katika kundi
moja kwa ajili ya kukiwezesha Chama kushinda na kuendeleza pale
walipoishia viongozi wa awamu ya kwanza hadi ya nne na yaliyobaki
yapatikane kwa haraka,” alifafanua.
Mgombea Mwenza kwa upande wake, Samia Suluhu Hassan, aliwataka
wana-Dar es Salaam kushikamana kwa kuwa umoja ni ushindi na kwamba Dk.
Magufuli ni tingatinga.
KINANA:TUTATENDA HAKI
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alisema chama hicho kimetimiza
50 kwa 50 kabla ya Katiba inayopendekezwa kwa kuweka mgombea urais
mwanaume na mgombea mwenza ambaye atakuwa Makamu wa Rais ni mwanamke.
0 comments:
Post a Comment